Ujumbe wa Msaada wa Umoja wa Mataifa nchini Libya (UNSMIL) umekana kile ulichokiita “madai” yasiyo ya kweli kuhusu kuwepo mpango wa umoja huo za kuwapa makazi wahamiaji ndani ya Libya, ukisisitiza kwamba madai haya “hayana msingi”.

Taarifa hii ya Umoja wa Mataifa iimetolewa kufuatia maandamano yaliyofanyika katika mji mkuu wa Libya, Tripoli, mbele ya ofisi za Umoja wa Mataifa.

Ujumbe huo umesema kwamba umefuatilia maandamano yaliyoandaliwa mbele ya makao yake ya Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Wakimbizi huko Tripoli, ukisisitiza haki ya Walibya kupata taarifa sahihi na kutoa maoni yao kwa amani, kwa mujibu wa sheria za kitaifa na mikataba ya kimataifa.

Ujumbe huo umeeleza wasiwasi wake kuhusu kuenea taarifa potofu na matamshi ya chuki yanayohusiana na kazi ya Umoja wa Mataifa nchini Libya, ikizingatiwa kwamba suala hilo limechangia kuongezeka mvutano na uchochezi dhidi ya wafanyakazi wa shirika hilo, wa Libya na wa kimataifa.

Taarifa ya UNSMIL imesisitiza kwamba mashirika ya Umoja wa Mataifa yanayofanya kazi nchini Libya – ikiwa ni pamoja na UNHCR – hayatekelezi programu zozote zinazolenga kuwapa makazi wahamiaji katika ardhi ya Libya.

Imeeleza kwamba kazi ya Tume inalenga – kwa ushirikiano na mamlaka ya Libya na jamii ya kimataifa – kutafuta suluhisho nje ya Libya kwa watu wanaokimbia vita, migogoro na mateso, ikiwa ni pamoja na kuhamishiwa kwenye nchi ya tatu au kuwezesha kurudi kwa hiari katika nchi zao za asili wakati hali inaporuhusu.

UNSMIL imelaani uchochezi wowote wa vurugu au vitisho vinavyowalenga wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa, pamoja na vitendo vya hujuma au mashambulizi kwenye majengo na mali yake, ikitoa wito kwa pande zote kuheshimu vifaa na wafanyakazi wa shirika hilo kwa mujibu wa sheria za kimataifa.

Pia imepongeza juhudi za mamlaka husika mjini Tripoli za kudumisha utulivu wa umma na kuhakikisha usalama wa waandamanaji, wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa, na vifaa vyake.

Mamia ya waandamanaji walikusanyika mbele ya makao makuu ya UNHCR katika wilaya ya Al-Sarraj mjini Tripoli, wakitoa kaulimbiu zinazopinga kile walichokielezea kama “makazi” ya wahamiaji nchini Libya, na kutaka kuondolewa kwao nchini humo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *