
Katika mahojiano na chombo cha habari cha Marekani Axios, Rais Doland Trump wa Marekani amekiri hadharani kwamba hakuwa na budi ila kufanya mazungumzo na Iran kwa ajili ya kumaliza vita.
Trump kwa mara nyingine tena ameashiria hofu yake ya kupungua akiba ya mafuta duniani kutokana na kuendelea vita dhidi ya Iran na kusema: ‘Lau tungeendelea kuishambulia Iran kwa mabomu, tungeshuhudia kufungwa kabisa hivi sasa kwa Lango Bahari la Hormuz.
Amesema: “Mabomu ya majini yalikuwa yanategwa katika eneo zima la Hormuz, makombora yakiruka juu ya meli za mabilioni ya dola ambazo hazikuthubutu kufanya harakati yoyote, na tulikuwa katika hatari ya kukosa mafuta kwa miezi.”
Huku akiwajibu wakosoaji wake wa Marekani ambao wanadai alipaswa kukabiliana vikali zaidi za Iran na kuendeleza vita, amesema: “Njia pekee ambayo ningeweza kuwa mkali zaidi ilikuwa ni kwenda huko kwa wiki mbili au tatu na kuendelea kuwashambulia kwa mabomu, sivyo? Lakini hilo lingekuwa na faida gani kwetu? Lango Bahari la Hormuz halingefunguliwa.”
Ameongeza: “Hatutakuwa na mafuta kwa miezi.” “Madamu mabomu yanaendelea kurushwa, lango hilo litaendelea kufungwa moja kwa moja, na hilo linaweza kusababisha mdororo wa uchumi.”
Takwimu za akiba ya mafuta ya Marekani zinaonyesha kuwa nchi hiyo bado iko katika hatari ya kukumbwa na mzozo wa mafuta. Hifadhi ya mafuta yasiyosafishwa katika kituo kikubwa zaidi cha kuhifadhi mafuta ya kibiashara nchini Marekani, cha Cushing, katika jimbo la Oklahoma, ambapo bei ya mafuta huainishwa, imeshuka hadi mapipa milioni 20, kiwango cha chini kabisa katika miaka 11 iliyopita.
Hifadhi ya Kimkakati ya Mafuta, ambayo ilibuniwa kwa ajili ya kusimamia usambazaji wa mafuta duniani, pia imeshuka hadi kufikia kiwango cha chini kabisa cha mapipa milioni 340.
Ni zaidi ya mwezi mmoja sasa ambapo wakurugenzi wa makampuni makubwa ya mafuta ya Marekani wamekuwa wakionya kwamba kufikia mwishoni mwa Juni au mwanzoni mwa Julai, akiba ya mafuta ya Marekani itafikia hatua ya mvutano wa kioperesheni, ikimaanisha kuwa hawataweza tena kufidia uhaba wa mafuta.