Dar es Salaam. Katika miaka ya hivi karibuni, ndoa na uhusiano vimepoteza faragha yake ya asili. Yaliyokuwa mambo ya ndani ya wanandoa sasa yamekuwa gumzo la vijiwe, mitandao ya kijamii na hata meza za kahawa. 

Kila anayesikia mgogoro anajiona ana haki ya kutoa ushauri, bila kujali anaelewa kwa kiasi gani mizizi ya tatizo. Hali hii imegeuza ndoa kuwa kama mali ya umma, jambo linaloleta madhara makubwa kuliko faida.

Mtaalamu wa masuala ya ndoa, Gary Chapman, anasisitiza kuwa kila ndoa ina mazingira yake, historia yake na mawasiliano yake ya kipekee. 

Kwa tafsiri ya mawazo yake, anabainisha kuwa kuiga ushauri wa ndoa ya mtu mwingine bila kuzingatia hali yako ni sawa na kuvaa viatu visivyokutosha. Chapman anaonya kwa maneno haya: “Mwenza wako si wa mtu mwingine. Kinachofanya kazi katika ndoa moja kinaweza kuharibu ndoa nyingine.”

 Kauli hii inaweka wazi ukweli kwamba si kila ushauri unaofaa kusikilizwa. Katika jamii zetu, kauli kama “achana naye mapema”, “usivumilie”, au “wanawake wote ni wale wale” zimekuwa rahisi kutamkwa. 

Ushauri huu hutolewa bila kujali athari zake za muda mrefu. Mara nyingi hutokana na maumivu ya walioumia awali, si kwa busara ya kujenga. Ndoa nyingi zimeharibika si kwa sababu matatizo yalikuwa makubwa, bali kwa sababu kelele za nje zilikuwa nyingi kuliko sauti ya busara ya ndani.

Hata maandiko ya dini yanatukumbusha hatari ya kusikiliza kila sauti. Mithali 19:27 inasema: “Acha kusikiliza maonyo, mwanangu, nawe utapotea kutoka katika maneno ya maarifa.” Hii si amri ya kukataa ushauri wote, bali ni onyo dhidi ya kusikiliza maelekezo yasiyo na hekima na mwelekeo.

Ushauri mwingi unavuruga

Mwandishi na mhamasishaji wa masuala ya uhusiano, Steve Harvey, anaonya kuwa watu wengi huingiza marafiki na ndugu kupita kiasi katika uhusiano wao. 

Kwa tafsiri ya mawazo yake, anasema kuwa mara nyingi washauri hawa hawabebi gharama ya uamuzi wanaopendekeza. 

Anasisitiza kwa maneno haya: “Watu wengi sana wanawaingiza watu wa nje katika uhusiano wao, na watu hao wa nje hawalipi gharama mambo yanapoharibika.”

Ni ukweli usiopingika kwamba mshauri anaweza kuondoka na kuendelea na maisha yake, lakini wanandoa hubaki na maumivu, lawama na wakati mwingine talaka. 

Ushauri wa hasira unaweza kutolewa kwa dakika tano, lakini madhara yake yakadumu maisha yote.

Ndiyo maana si kila anayesikiliza simulizi yako anapaswa kupewa nafasi ya kukuongoza.

Katika mila za Kiafrika, wazee walikuwa wakitoa ushauri wa ndoa kwa umakini mkubwa na kwa siri. Leo, nafasi hiyo imechukuliwa na watu wengi wasio na subira wala uzoefu.

Kila ndugu anataka kutoa kauli, kila rafiki anataka kusikika. Matokeo yake ni mgongano wa ushauri unaowaacha wanandoa wakichanganyikiwa, wakikosa mwelekeo sahihi.

Mtafiti wa masuala ya ndoa, John Gottman, ambaye amechunguza ndoa nyingi kwa miaka mingi, anaeleza kuwa ushawishi hasi kutoka nje unaweza kuwa hatari zaidi kuliko migogoro ya wanandoa wenyewe.

Anasema: “Mshawasha hasi kutoka nje unaweza kuharibu ndoa kwa kasi zaidi kuliko migogoro ya ndani.” Kauli hii inaonyesha wazi kuwa kelele za watu zinaweza kuharibu msingi wa ndoa haraka sana.

Kwa mujibu wa tafsiri ya mawazo yake, Gottman anaamini kuwa wanandoa wanaojifunza kukabiliana na changamoto zao kwa faragha, kwa heshima na kwa mawasiliano ya wazi, wana nafasi kubwa ya kudumisha ndoa zao kuliko wale wanaokimbilia kwa kila mtu wanapokumbwa na tatizo.

Hekima ya kuchagua mshauri

Kuepuka washauri wengi hakumaanishi kukataa msaada kabisa. Badala yake, ni kuchagua kwa makini nani wa kumsikiliza. 

Mwandishi na mchungaji Timothy Keller anaeleza kuwa ndoa imara hujengwa kwa ushauri wa wachache wenye hekima, si kwa kelele za wengi. Anasema: “Ndoa bora haijengwi na sauti nyingi, bali na sauti chache zenye hekima na uaminifu.”

Anaeleza kuwa mshauri mzuri ni yule anayelinda thamani ya ndoa, anayehimiza uvumilivu, mazungumzo na ukuaji wa pamoja.

 Si yule anayechochea uamuzi wa haraka au anayefurahia kuona ndoa ikivunjika. Ushauri wa aina hii unahitaji mtu mwenye uzoefu, maadili na moyo wa kweli wa kusaidia.

Ndoa si mahali pa majaribio ya mawazo ya watu wengi. Ni safari ya watu wawili wanaojifunza kila siku. Kusikiliza kila mtu ni sawa na kuendesha gari lenye madereva wengi; mwisho wake ni ajali isiyoepukika.

Kumbuka kuwa kelele huleta mkanganyiko, lakini hekima huleta mwelekeo. Jamii inapaswa kujifunza kuheshimu mipaka ya ndoa za wengine, na wanandoa wajifunze kulinda faragha yao.  Ndoa yako inahitaji amani, si makelele ya watu; inahitaji ujenzi wa pamoja, si 

uamuzi unaochochewa na hisia za wengine. Makala haya kwa hisani ya vyanzo mbalimbali vya kimtandao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *