Dar es Salaam. Mjadala kuhusu marekebisho ya Sheria ya Fedha 2026 yanayoruhusu Serikali kukopeshwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) umeendelea kugawa maoni ya wadau, huku baadhi wakidai kifungu kipya hakijaeleza namna mkopo huo utakavyorejeshwa.

Wengine wanahoji, inawezekanaje Serikali ijikopeshe akiba zake, wakifafanua fedha zilizopo BoT ni akiba na ina mamlaka ya kuzitumia inapotokea dharura.

Kiini cha mjadala huo ni kifungu kipya cha 69 kinachoruhusu BoT kuipatia Serikali mkopo wa muda mfupi, endapo kutatokea tukio lisilotarajiwa au lisiloepukika linalosababisha upungufu wa muda wa mapato ya Serikali.

Kifungu hicho cha 69(1) kinasema, “kwa kuzingatia masharti ya vifungu vya 34, 35 na 37, benki hiyo inaweza kuipa Serikali mkopo wa muda mfupi pale panapotokea tukio lisilotarajiwa au lisiloepukika linalosababisha upungufu wa muda wa mapato ya Serikali.”

Kifungu cha 69(3) a hadi c, kinaeleza “Kwa madhumuni ya kifungu hiki, tukio lisilotarajiwa au lisiloepukika litahusisha tu, janga kama lilivyofafanuliwa katika Sheria ya Usimamizi wa Maafa.”

Pia, kinahusisha tukio, hali au sababu ya kiuchumi kutoka nje ya nchi yenye ukubwa na athari za kipekee na hali ya hatari iliyotangazwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kuhusu urejeshaji wa mkopo

Katika mitandao ya kijamii, wadau mbalimbali wameyapinga marekebisho hayo, wakisema yameipa Serikali mwanya wa kujikopesha BoT, bila kuweka wazi mpango wa marejesho ya mkopo huo.

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X, Wakili wa Kujitegemea, Jebra Kambole ameandika kuwa, kwa inavyoonekana, Serikali inataka kuikopa BoT na haikuweka njia za kurejesha fedha hizo.

“Mapendekezo ya marekebisho ya sheria, Serikali wanataka kuwa wanakopa BoT na hakuna njia za kisheria za kurudisha fedha hizo,” ameandika Kambole.

Kwa mtazamo wake, hiyo ni namna nyingine ya kuitafuna nchi, watu wamekosa pa kukopa, wanaamua kuanza kujikopesha bila kulipa.

Hata hivyo, uchambuzi wa sheria unaonesha suala la Serikali kurejesha mkopo huo limeainishwa katika vifungu vya 34, 35 na 37 vya Sheria ya BoT vinavyorejelewa na kifungu cha 69 cha Sheria ya Fedha kilichorekebishwa.

Kwa mujibu wa kifungu cha 34(2)(a) cha Sheria ya BoT, Serikali itatakiwa kurejesha mkopo huo ndani ya siku 180. Takriban miezi sita tangu muda wa kutolewa kwake.

Aidha, kifungu cha 34(2)(b) kinaeleza kuwa mkopo huo, “utatozwa riba kwa viwango vya soko vitakavyowekwa na benki.”

Kwa upande wa kifungu cha 35, kimeweka ukomo wa fedha ambazo Benki Kuu inaweza kuikopesha Serikali kupitia mikopo na dhamana mbalimbali kutoka asilimia 18 hadi 14 ya mapato ya mwaka uliopita.

Kifungu cha 37, kinasema isipokuwa kwa yale yaliyotajwa kwenye vifungu 34 na 35, Benki Kuu hairuhusiwi kuikopesha Serikali moja kwa moja wala kwa njia nyingine yoyote.

Kujikopesha

Jana Jumatatu, Juni 22, 2026 Mchambuzi wa Sera za Fedha, Dk Leonard Rweyemamu amesema pamoja na kuwepo kwa masharti ya kisheria, hatua ya Serikali kutegemea mikopo kutoka BoT inaweza kuathiri nidhamu ya fedha za umma na uhuru wa taasisi hiyo.

Amesema moja ya majukumu makuu ya BoT ni kulinda thamani ya fedha, kudhibiti mfumuko wa bei na kuhifadhi akiba za Taifa.

“Kadiri Serikali inavyopata urahisi wa kukopa BoT, ndivyo hatari ya kubweteka kwenye kuboresha ukusanyaji wa mapato na usimamizi wa matumizi ya umma inavyoongezeka,” amesema Dk Rweyemamu.

Jambo muhimu, amesema si uwezo wa Serikali kupata fedha wakati wa dharura, bali kuhakikisha utaratibu huo haugeuki kuwa tegemeo la kudumu.

“Serikali zinapoanza kutegemea fedha za benki kuu, kunaathiri uhuru wa sera za fedha na kuongeza hatari ya mfumuko wa bei endapo hakutakuwa na udhibiti,” amesema.

Kwa upande wake, Mchambuzi wa Uchumi, Profesa Amani Mshana amesema katika nchi nyingi, benki kuu hutoa mikopo ya muda mfupi kwa Serikali wakati wa mishtuko ya kiuchumi, majanga au changamoto za muda za mtiririko wa mapato.

“Kwa kuwa sheria imeweka ukomo wa kiasi kinachoweza kukopwa, muda wa kurejesha na riba ya soko, basi kiuchumi utaratibu huo utaisaidia Serikali kukabiliana na mishtuko ya muda bila kulazimika kukopa katika masoko ya fedha ya ndani au nje ya nchi yenye gharama kubwa,” amesema.

Akizungumzia hilo, Mtaalamu wa Uchumi, Dk Isdori Minani amesema ingekuwa kawaida kama kungelikuwa na uadilifu na uwajibikaji katika usimamizi wa fedha hizo zinazokopwa.

Lakini, changamoto ya uadilifu na kukosekana uhuru wa taasisi za usimamizi, amesema zinatengeneza hofu iwapo fedha hizo zitakazokopwa zitarejeshwa na Serikali.

“Kama viongozi wa nchi husika ni waadilifu, kuna usimamizi na kuna uhuru wa taasisi wa kuisimamia Serikali kwamba imekopa na inatakiwa kurudisha, hili lingekuwa jambo jema,” amesema Dk Minani.

Amesema shaka lake kuhusu uadilifu na uwajibikaji, linatokana na mara kadhaa Serikali ikishuhudiwa kukopa kwenye mifuko ya hifadhi za jamii na kuchelewa kulipa, hivyo kusababisha mifuko kuyumba na wastaafu kucheleweshewa mafao yao.

 Amesema kufaa au kutofaa kwa utaratibu huo kunategemea uadilifu wa Serikali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *