Dar es Salaam. Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) imewataka wadau mbalimbali wakiwamo wazalishaji wa teknolojia za nishati safi kutoa mapendekezo yatakayosaidia kufanyika kwa maboresho katika sera na mifumo ya kodi ili kuchochea ukuaji wa sekta hiyo nchini.

Wito huo umetolewa leo Alhamisi, Juni 25, 2026 katika mjadala ulioandaliwa na TPSF kwa kushirikiana na Kampuni ya Kengo Limited na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Mitaji (UNCDF), uliolenga kujadili utekelezaji wa bajeti ya mwaka huu na mchango wake katika maendeleo ya sekta ya nishati safi nchini.

Akizungumza katika mjadala huo, Meneja wa Utafiti, Sera na Ushawishi wa TPSF, Mercy Philipo amesema sekta binafsi inaendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali pamoja na wadau wengine kuhakikisha lengo la asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati safi ifikapo mwaka 2034 linafikiwa.

Amesema maoni na mapendekezo ya wadau ni muhimu katika kufanikisha azma hiyo, hasa katika kubaini maeneo yanayohitaji maboresho ili kuweka mazingira bora kwa wazalishaji wa teknolojia za nishati safi na watumiaji wake.

 Inakadiriwa asilimia 28 ya Watanzania wanatumia nishati sasa kwa sasa.

“TPSF kwa niaba ya sekta binafsi, ni mjumbe wa kamati ya mawasilisho ya maoni ambayo hukutana Oktoba kila mwaka. Hivyo ni muhimu kwa wadau kutoa mapendekezo ya maeneo wanayotaka Serikali iyafanyie kazi ili sekta ya nishati safi iwe rafiki zaidi kwa wawekezaji, wazalishaji na watumiaji,” amesema Philipo.

Amesema Serikali imeonesha usikivu kwa baadhi ya maombi yaliyowasilishwa na sekta binafsi, ikiwamo kuondoa ushuru kwenye vifaa vya kusoma matumizi ya gesi hatua ambayo imechangia kupunguza gharama katika sekta hiyo.

“Tunaishukuru Serikali kwa kuondoa ushuru katika baadhi ya maeneo tuliyopendekeza. Hata hivyo, bado kuna maeneo mengine, ikiwamo vifuniko vya gesi, ambavyo tumeomba navyo vipewe unafuu wa kodi ili kupunguza gharama kwa watumiaji,” amesema.

wadau wa nishati safi kutoka sekta binafsi wakiwa katika picha ya pamoja baada ya majadiliano yanayoendana na bajeti ya mwaka huu kuhusiana na nishati safi yaliyoandaliwa kwa pamoja na Taasisi ya Sekta Binafsi nchini ( TPSF), Kengo Limited na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo la Mitaji ( UNCDF) jijini Dar es Salaam jana

Akiwasilisha mapendekezo ya sekta binafsi, Philipo ametaja maeneo ya kipaumbele ni pamoja na kupunguza gharama za vifaa vinavyotumika katika matumizi ya nishati safi ili kuongeza hamasa kwa wananchi kutumia teknolojia hizo.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha uwekezaji katika viwanda vya ndani vinavyozalisha vifaa vya nishati safi, ikiwamo majiko ya kisasa, hatua ambayo alisema itasaidia kukuza uchumi wa nchi na kuongeza ajira.

Pia, ameeleza umuhimu wa kuwepo kwa mfumo madhubuti wa usambazaji wa teknolojia za nishati safi ili kuhakikisha zinawafikia wananchi wengi zaidi, hususan wanaoishi maeneo ya vijijini.

Kwa upande wake, Rehema Mbalamwezi kutoka Kampuni ya UpEnergy amesema elimu kwa umma inapaswa kupewa kipaumbele ili kuongeza uelewa na hamasa ya matumizi ya nishati safi na mbadala, hatua itakayosaidia kupunguza utegemezi wa mkaa na kuni.

Ametolea mfano Mkoa wa Dar es Salaam akisema idadi kubwa ya wakazi bado wanategemea mkaa kama chanzo kikuu cha nishati ya kupikia.

Mbalamwezi ametoa wito wa kuongezwa kwa uwekezaji katika viwanda vinavyozalisha vifaa vya kisasa vya nishati safi, hususan vinavyotumia umeme, akieleza nishati hiyo ni nafuu na rafiki kwa mazingira, lakini bado haijapewa kipaumbele kinachostahili katika matumizi ya kila siku ya wananchi.

Kwa upande wake, mdau wa sekta hiyo, Sylvester Mwambije, amesema pamoja na umuhimu wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi na mbadala, kuna haja ya kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi salama na bora ya nishati za asili ambazo kwa kiasi kikubwa ndizo wanazotumia kwa sasa.

“Tunaelezwa kuwa matumizi ya mkaa na kuni yana madhara kwa mazingira na afya. Hata hivyo, wakati tunaendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi, ni muhimu pia kuwapatia wananchi elimu kuhusu namna ya kuboresha matumizi ya nishati za asili na kupunguza athari zake,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *