
Wizara ya Mambo ya Nje ya Yemen mjini Sana’a imelaani vikali shambulio la Saudi Arabia dhidi ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Sana’a, ikisisitiza kuwa hatua hiyo ya kijeshi inahitimisha rasmi kipindi cha usitishaji vita na kuashiria kuanza kwa awamu mpya ya vita.
Katika taarifa iliyotolewa siku ya Jumatatu, wizara hiyo ilitangaza kuwa Yemen itaingia katika hatua mpya ya kutetea haki zake zote kwa ukamilifu, huku ikiionya Saudi Arabia kuwa itajikuta katika mkwamo mkubwa wa kimkakati na italazimika kulipa gharama kubwa kwa uvamizi wake.
Katika hatua nyingine, Msemaji wa Majeshi ya Yemen, Jenerali wa Brigedia Yahya Saree, ameonya kuwa “uvamizi wa Saudi hautapita bila malipo,” akiongeza kuwa, “Adui Msaudi amehitimisha awamu ya kupunguza mivutano, na ni lazima abebe dhima ya matokeo yote yanayoweza kufuata.”
Wizara ya Uchukuzi ya Yemen ilitangaza kupitia taarifa yake kuwa “shambulio la mabomu la Saudi Arabia dhidi ya uwanja wa ndege wa Sana’a na ukiukaji wa anga ya Yemen ni dhihirisho la msisitizo wa utawala wa Riyadh, kwa uchochezi wa Marekani na Wazayuni, kuendeleza mzingiro dhidi ya watu wa Yemen.”
Aidha, chanzo cha ngazi ya juu nchini Yemen kimebainisha kuwa “uamuzi wa kuvunja mzingiro wa uwanja wa ndege wa Sana’a hauwezi kubadilika,” akielezea utayari wa hali ya juu wa kivita wa Majeshi ya Yemen na maandalizi yao kwa ajili ya hali yoyote ile inayoweza kujitokeza.
Chanzo hicho kilisisitiza kuwa Saudi Arabia ndiyo inayohusika na kukwamisha juhudi za kurejesha amani na utulivu kote Yemen. Chanzo hicho kimebaini kuwa: “Viongozi wa Saudi hawana uelewa mpana wa hali halisi ilivyo sasa, na wanategemea tu mamluki wa utawala huo kufanya maamuzi ya kukurupuka.”
Mwishoni, chanzo hicho kilionya kuwa uchumi wa Saudi Arabia, viwanja vyake vya ndege, na bandari zake zitalazimika kubeba mzigo mzito wa athari za uwendawazimu wowote utakaofanywa na Riyadh.