
Saa chache baada ya kusambaa kwa taarifa za kutekwa kwa mwanasiasa huyo, aliyewahi kushikilia nafasi mbalimbali serikalini na kwenye chama tawala cha CCM, Jeshi la Polisi limesema kuwa tayari limeanza kufanya uchunguzi wa madai ya kutekwa au kupotea kwake.
Jeshi hilo limesema, awali walikuwa wakimtafuta Polepole ili aweze kuwasaidia kuhusiana na tuhuma mbalimbali ambazo amekuwa akizitoa na limesisitiza kuwa wanafanyia uchunguzi taarifa za kutekwa kwake.
Leo asubuhi taarifa za kutoweka kwa Polepole zilisambaa kupitia mitandao ya kijamii huku zikionyesha nyumba inayodaiwa kuwa ni makaazi ya Polepole, ikiwa imeharibiwa na kuonekana kwa alama za damu sakafuni.
Kaka wa Polepole azungumza na DW
Kaka wa Polepole, Godfrey Polepole alipozungumza na DW amesema mara ya mwisho kuzungumza na kaka yake ilikuwa siku ya Jumapili majira ya saa 2 za usiku na kusema alimsisitiza kuwa makini kwani kama familia wamekuwa wakifuatiliwa na kumuonya kuacha kutembea usiku.
Polepole, ambaye pia aliwahi kuwa katibu mwenezi na itikadi wa CCM na ambaye katika siku za karibuni amekuwa mkosoaji mkubwa wa serikali amewahi pia kuwa mbunge na Balozi wa Tanzania nchini Malawi na kabla ya kujiuzulu, alikuwa balozi wa Tanzania nchini Cuba akiiwakilisha Tanzania katika visiwa vya Karibiani, Amerika ya Kati, Columbia na Guyana.