Merz kuongoza mkutano wa dharura kuhusu sekta ya magariMerz kuongoza mkutano wa dharura kuhusu sekta ya magari

Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz anatarajiwa Alhamisi kuongoza kikao cha dharura na viongozi wa sekta ya magari nchini humo, kujadili mustakabali wa sekta hiyo muhimu inayokabiliwa na changamoto nyingi — kutoka marufuku ya injini za mwako barani Ulaya hadi ushindani mkali kutoka China.

Kwa miongo mingi, sekta ya magari iliyoongozwa na makampuni makubwa kama Volkswagen, BMW na Mercedes-Benz imekuwa nguzo kuu ya uchumi wa Ujerumani. Lakini sasa inakabiliwa na kipindi kigumu chenye kupungua kwa mauzo, hasara kubwa na wimbi la kupunguza wafanyakazi.

Sekta inayoyumba

Kampuni nyingi za magari na wasambazaji wa vipuri zinahangaika kutokana na mabadiliko ya polepole kuelekea magari ya umeme, pamoja na ushindani mkali kutoka kwa watengenezaji wa magari ya umeme wa China na sera kali za ushuru za Rais wa Marekani, Donald Trump.

Kwa mujibu wa msemaji wa serikali, Steffen Meyer, mazungumzo hayo yanalenga “kutafuta njia ya mbele kwa sekta ambayo ni muhimu sana kwa ustawi na ajira za Wajerumani.”

Ujerumani Berlin 2025 | Mkutano wa Baraza la Mawaziri ukiwahusisha Lars Klingbeil, Dorothee Bär na Friedrich Merz
Kansela Friedrich Merz (kulia) na naibu wake ambaye ni waziri wa fedha Lars Klingbeil wataongoza kikao na wadau wa sekta ya magari ya Ujerumani.Picha: Ulrich Stamm/Geisler-Fotopress/picture alliance

Kikao hicho cha saa mbili katika Ukumbi wa Kansela mjini Berlin kitawakutanisha viongozi wa viwanda vya magari, mawaziri wa serikali na wawakilishi wa vyama vya wafanyakazi.

Baada ya majadiliano, Merz, Waziri wa Fedha Lars Klingbeil, na viongozi wa VDA (shirikisho la magari) pamoja na IG Metall wanatarajiwa kutoa tamko kwa vyombo vya habari saa nane alasiri kwa saa za Berlin.

Mvutano kuhusu injini za mwako

Kati ya mambo makubwa yatakayojadiliwa ni mpango wa Umoja wa Ulaya wa kukomesha uuzaji wa magari mapya yenye injini za mwako kufikia mwaka 2035 katika juhudi za kupunguza uzalishaji wa gesi chafu.

Wazalishaji wa magari wa Ujerumani wamepinga mpango huo wakihofia utayumba biashara zao, hasa kwa kuwa mabadiliko kuelekea magari ya umeme yanasuasua. Hata hivyo, EU imeahidi kufanya mapitio ya haraka ya sera hiyo kufuatia malalamiko hayo.

Merz, kutoka chama cha CDU, ameendelea kushinikiza kufutwa kwa mpango huo kabisa akisema “ni maamuzi yasiyo sahihi.” Kauli hiyo imezua mivutano na washirika wake wa muungano wa SPD, ambao wanataka tarehe ya marufuku ibaki kama ilivyopangwa.

Vyombo vya habari vya Ujerumani vimeripoti kuwa serikali inaweza kutafuta muafaka wa kati – wa kupunguza ukali wa marufuku bila kuiondoa kabisa.

Viwanda vya magari Ujerumani kutumia malighafi za taka

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Pendekezo la kodi na chuma rafiki wa mazingira

Pendekezo jingine mezani ni la Waziri wa Fedha Klingbeil, ambaye anataka serikali kuongeza muda wa punguzo la kodi kwa magari ya umeme hadi mwaka 2031, ili kuhimiza mpito wa umeme.

Gazeti la Handelsblatt limeripoti kuwa serikali pia inatafakari kuruhusu watengenezaji wa magari wanaotumia “chuma kijani” kilichozalishwa Ulaya kuwa na malengo mepesi zaidi ya kupunguza CO₂. Hata hivyo, hatua hiyo inahitaji idhini ya Umoja wa Ulaya.

Mtaalamu wa sekta ya magari kutoka Chuo Kikuu cha FHM mjini Cologne, Frank Schwope, ameiambia AFP kuwa haoni matarajio makubwa ya kutolewa kwa tangazo lolote lenye uzito kutoka kikao hicho.

“Kunaweza kuwa na ahadi ndogo ndogo, kama uwekezaji katika utafiti wa betri,” alisema, “lakini wengi watajadili sana na kuamua kidogo — kwa sababu maamuzi makubwa hufanywa katika ngazi ya Ulaya.”

Chanzo: AFP

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *