Mchujo huo wa awali unasaka timu moja ya Afrika ambayo itaingia katika hatua ya mwishi ya mchujo ambayo itahusisha timu sita kutoka mabara matano tofauti duniani na imepangwa itachezwa Machi mwakani.

Rabat, Morocco. Macho, masikio na hisia za mamilioni ya mashabiki wa soka Afrika zinaelekezwa Rabat, Morocco ambako leo kunachezwa mechi mbili za nusu fainali ya hatua ya mchujo wa awali wa kusaka tiketi ya Fainali za Kombe la Dunia 2026.

Mchujo huo wa awali unasaka timu moja ya Afrika ambayo itaingia katika hatua ya mwishi ya mchujo ambayo itahusisha timu sita kutoka mabara matano tofauti duniani na imepangwa itachezwa Machi mwakani.

Ni hatua inayoshirikisha timu nne ambazo zilimaliza katika nafasi ya pili zikiwa na matokeo mazuri kwenye hatua ya makundi ya kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2026 ambayo ilitoa timu tisa zilizofuzu moja kwa moja fainali hizo ambazo zitafanyika Marekani, Canada na Mexico.

Mechi mbili zitakazochezwa leo chini ya usimamizi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) ni kati ya Gabon na Nigeria na mwingine ni baina ya DR Congo na Cameroon.

Gabon na Nigeria ndio zitafungua dimba ambapo zitakutana katika Uwanja wa Moulay Hassan kuanzia saa 1:00 usiku kwa muda wa Tanzania.

Ni mchezo unaokutanisha timu mbili ambazo zimeonyesha makali ya kufumania nyavu katika hatua ya makundi ambapo Gabon ilifunga mabao 22 sawa na wastani wa mabao 2.2 kwa mchezo huku Nigeria ilipachika mabao 15 ikiwa ni wastani wa bao 1.5 kwa mechi.

Nigeria ilimaliza katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi C ikiwa na pointi 17 na Gabon ilimaliza katika nafasi kama hiyo kwenye kundi F ikiwa na pointi 25.

Siku mbili kabla ya mechi hiyo, iliripotiwa kwamba wachezaji wa Nigeria walitangaza mgomo kwa ajili ya kushinikiza malipo ya madai yao ya muda mrefu ya posho na bonasi za ushindi wa mechi mbalimbali ingawa baadaye mgomo huo ulimalizwa.

Mechi hiyo ya Nigeria na Gabon itachezeshwa na refa Tom Abongile kutoka Afrika Kusini akisaidiwa na Jerson Santos wa Angola na msaidizi wa pili akiwa ni Zakhele Siwela kutoka Afrika Kusini na refa wa akiba ni L Ahmad Imtehaz.

Mchezo wa pili ambao utazikutanisha DR Congo na Cameroon, utachezwa kwenye Uwanja wa Al Barid kuanzia saa 4:00 usiku.

DR Congo ilimaliza katika nafasi ya pili kwenye kundi B ikiwa na pointi 22 na Cameroon ilimaliza ikiwa na pointi 19 katika kundi D.

Kuna habari njema katika kambi ya DR Congo ambayo inaweza kuipa morali zaidi timu hiyo katika mechi ya leo.

Habari ni ahadi ya Dola 1 milioni (Sh2.5 bilioni) kwa kila mtu aliyepo kwenye kikosi cha timu ya taifa ya nchi hiyo ikiwa itapata ushindi dhidi ya Cameroon.

Lengo la serikali ya DR Congo ni kuongeza hamasa kwa wachezaji wa timu hiyo ili kuhakikisha inafanya vizuri na kutinga hatua ya fainali.

Mechi hiyo baina ya Cameroon na DR Congo itachezeshwa na Refa Dahane Beida kutoka Mauritania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *