
Katika taarifa, Rais Paudel amewahimiza raia kuwa watulivu na kuonyesha umoja kwa ajili ya kupata suluhisho la amani baada ya waandamanaji kuchoma moto majengo ya bunge pamoja na ofisi ya rais.
Wito huo ameutoa saa chache baada ya Waziri Mkuu Sharma Oli kujiuzulu.
Licha ya kujiuzulu kwa Waziri Mkuu huyo, maandamano bado yanaendelea nchini humo. Maelfu ya waandamanaji, wengi wao vijana, wamefurika mitaani na kufunga barabara, kuvamia majengo ya serikali na kuyachoma moto na hata kushambulia baadhi ya viongozi wa kisiasa. Helikopta za kijeshi zinaripotiwa kuwaokoa mawaziri kadhaa na kuwapeleka maeneo salama.
Mapema jana, kulifanyika maandamano mjini Kathmandu yaliyoongozwa na vijana, wakipinga kukandamizwa kwa uhuru wa kujieleza mtandaoni na ufisadi serikali.
Takriban watu 19 wamefariki na zaidi ya 100 wamejeruhiwa katika ghasia hizo, ambazo zinatajwa kuwa mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini Nepal katika miaka ya hivi karibuni.