Televisheni ya CNN ya Marekani imeripoti kuwa, Saudi Arabia imetoa tuhuma zisizo za kawaida dhidi ya Muungano wa Falme za Kiarabu, Imarati huku kukiwa tayari kuna mvutano unaoongezeka kati ya mataifa hayo mawili ya Ghuba ya Uajemi, tuhuma ambazo zinahusu wasiwasi kuhusu namna UAE inavyojihusisha na masuala ya Syria.

Kwa mujibu wa CNN, Riyadh inaamini kwamba Abu Dhabi “imepanda mbegu za uhusiano na vikundi vya jamii ya Wadruze wa Syria, ambavyo baadhi ya viongozi wao wamezungumzia waziwazi suala la jamii yao kujitenga na nchi hiyo.

CNN imesema, Saudi Arabia inaliona hilo kama tishio la moja kwa moja kwa umoja wa Syria na usalama wake wa taifa.

Chaneli hiyo ya televisheni imebainisha kuwa, wasiwasi wa Saudia kuhusu sera za Imarati nchini Syria ni sehemu ya mtazamo mpana ilionao kwamba kuunga mkono wadau wasio wa kiserikali katika eneo au kujihusisha na mipango nyeti ya ndani kunaweza kupelekea kuvurugika utulivu wa kikanda na kuanzisha mifano ya mienendo hatari itakayoathiri nchi jirani, hususan Saudi Arabia.

Ripoti hiyo ya CNN imeongeza kuwa tuhuma hizo za Saudi Arabia dhidi ya Muungano wa Falme za Kiarabu zilizotolewa waziwazi na hadharani ni ithibati ya kuwepo mpasuko mkubwa kati ya washirika hao wawili wa Ghuba ya Uajemi baada ya miaka mingi ya kuwepo uratibu na uhusiano wa karibu baina yao.

Lugha kali iliyotumiwa na Riyadh inaashiria wasiwasi wake unaoongezeka kuhusu sera za nje za Imarati ambayo inazidi kujichukulia hatua kivyake zisizoendana na mielekeo ya jadi ya kuwepo msimamo wa pamoja wa nchi za Kiarabu za kanda hii.

Kwa mujibu wa CNN, wasiwasi huo hauishii Syria pekee, bali umeenea hadi Yemen, Sudan, na Pembe ya Afrika. Huko Yemen, ambayo ina mpaka mrefu wa pamoja na Saudi Arabia, Riyadh inachelea athari za uungaji mkono wa Imarati kwa vikosi vya kusini vinavyotaka kujitenga na Yemen moja. Na huko Sudan, ambayo iko kwenye Bahari Nyekundu mkabala na pwani ya magharibi ya Saudi Arabia, kukosekana utulivu au kuanguka kwa serikali kunaweza kusababisha hatari za moja kwa moja kwa usalama wa taifa wa Saudia…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *