Chunya. Halmashauri ya Wilaya ya Chunya Mkoa wa Mbeya, imeweka mikakati ya kuwabana  wazazi na walezi watakao bainika kuwatumikisha watoto  kwenye kilimo cha  tumbaku na uchimbaji wa madini ya dhahabu.

Hatua hiyo imekuja ikiwa zimebaki siku mbili kufunguliwa kwa muhula mpya wa masomo 2026, sambamba na kutekeleza maagizo ya Serikali kuhakikisha watoto wote walio na umri wa kuanza masomo hususani wa walio chaguliwa kujiunga kidato cha kwanza wanapata elimu bila vikwazo.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Chunya, Athuman Bamba amesema hayo Januari 10, 2026,baada ya kuhojiwa na Mwananchi Digital namna  walivyo jipanga kudhibiti tabia ya baadhi ya wazazi kushiri kutumikisha watoto  kwenye vibarua vya kilimo cha tumbaku na uchimbaji wa madini badala ya kupata elimu.

Bamba ambaye pia  ni Mwanasheria Halmashauri hiyo,  amesema mwaka huu  wameweka mkazo wa kutumia sheria kwa wazazi ambao watazembea kwa makusudi na kusababisha watoto kuacha masomo na kutumikishwa shughuli za kilimo na uchimbaji wakati serikali imetumia fedha nyingi kuboresha miundombinu ya  elimu.

“Kwa wazazi ambao tutabaini kuzembea kusimamia elimu kwa watoto na badala yake kuwatumikisha kwenye mashamba ya tumbaku na uchimbaji wa madini watawajibishwa kwa mujibu wa kanuni na sheria kuanzia kwenye mabaraza ya Kata na Wilaya, “amesema.

Ataja sababu

Bamba ametaja miongoni mwa sababu ambazo zitawabana wazazi ni pamoja na uwekezaji wa serikali  miundombinu ya  elimu na maboresho ya shule shikizi maeneo ya pembezoni hususani kwa jamii ya wakulima na wafugaji.

“Miaka ya nyumba wazazi walikuwa wanataja umbali mrefu kufuata elimu ni chanzo watoto kuacha masomo  ,lakini sasa Serikali imejenga kila Kata na hakuna sababu ya mwanafunzi kukacha masomo bali mzazi atawajibishwa ,”amesema.

Amesema  katika kuhakikisha sera ya elimu inatekelezwa kwa vitendo  halmashauri kupitia mapato ya ndani imeboresha miundombinu  na kusajiri vituo shikizi 9,katika  maeneo ya pembezoni ya jamii ya wakulima na wafugaji ili kuondoa hadha ya watoto kutembea umbali mrefu kufuata elimu.

“Chunya tuna shule 90  tatu za watu  binafsi ,lakini za serikali 87, kati ya hizo shikizi ni shule 9, ambazo halmashauri imeboresha na kuzisajiri kwa ajili ya kupokea wanafunzi na kupelekea walimu ili kuhakikisha kila mtoto anapata elimu,”amesema.

Kuhusu uhakika wa chakula mashuleni

Amesema halmashauri imeweka mikakati ya kuchangia Sh 1,000 kwa kila mwanafunzi wa shule ya Msingi na Sekondari kupitia mapato ya ndani kwa ajili ya huduma ya chakula mashuleni lengo ni kuboresha kiwango cha taaluma.

Amesema zaidi ya Sh 450 milioni zimechangwa kutunusha  Mfuko wa Maendeleo Chunya,unao husisha wadau wa kilimo cha tumbaku na madini ya dhahabu kwa lengo la kuboresha sekta ya elimu wilayani humo.

Kuhusu makusanyo

Bamba amesema  wamekusudia kuvunja rekodi ya makusanyo ya mapato ya ndani kutoka Sh 10  bilioni za sasa hadi Sh 14 bilioni  kwa mwaka huu wa fedha huku asilimia 60 zitaelekezwa kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo.

Bamba ametaja miongoni mwa vyanzo vya vikubwa vya makusanyo ni pamoja na sekta ya kilimo na madini sambamba kutoa vitendea kazi na motisha ya asilimia10 kwa watendaji jambo ambalo linawapa morali ya kukusanya na kubuni vyanzo vipya.

Kwa upande wake Kaimu Ofisa Elimu Sekondari Wilaya ya Chunya, Lukelo Mng’on’go amesema kwa mwaka 2026, wanafunzi 4,132, wamechaguliwa kujiunga kidato cha kwanza huku 41 wamepangiwa nje ya Wilaya hiyo.

“Tunahamasisha wazazi ifijapo Januari 13, mwaka huu watoto wote walio chaguliwa kujiunga kidato kwanza wawe wameripoti mashuleni pasipo sababu yoyote ya kukosa sare za shule ,”amesema.

Naye Kaimu Ofisa Elimu Awali, Msingi Wilaya ya Chunya, John Gwimile amesema jumla ya watoto 12,478, wameandikishwa kuanza elimu ya msingi kati hao wanaume 6,207 sawa na asilimia 33.

Amesema pia halmashauri imetumia mapato ya ndani na fedha kutoka Serikali kuu kwa ajili ya ujenzi wa bweni la watoto wenye mahitaji maalum.

Kauli za wananchi

Mkazi wa Kiwanja, Salma Mohamed ameomba Serikali kuwekea mkazo suala la elimu kwa watoto kwa kudhibiti tamaa za wazazi kuwatumikisha au kuwasafirisha kwenda kufanya kazi za ndani mikoani.

“Miezi kama hii ya kuanza muhula wa masomo kuna baadhi ya wazazi hawaoni umuhimu wa kupeleka watoto kupata elimu na badala yake wamewageuza kitega uchumi kwa  kuangalia maslai ya fedha badala kutimiza ndoto za kupata elimu,”amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *