Dar es Salaam. Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), imezibwaga tena mahakamani Benki za Standard Chartered Hong Kong (SCBH) na Standard Chartered Bank Malaysia Berhad, katika rufaa ya usajili wa hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu ya Haki ya Uingereza, (Queen’s Bench Division – Commercial Court).

Katika hukumu hiyo iliyotokana na shauri la madai ya ukiukwaji mkataba wa mkopo uliotolewa na benki hizo kwa IPTL, Mahakama hiyo ya Uingireza iliiamuru IPTL kuzilipa benki hizo Dola za Marekani 168.8 zaidi ya Sh412.87 bilioni kwa kiwango cha ubadilishaji fedha Benki Kuu leo.

Baada ya kupata hukumu hiyo, benki hizo zilifanikiwa kuisajili hukumu hiyo Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Biashara, ili iweze kutekelezwa kwa mujibu wa sheria za Tanzania.

Hata hivyo baadaye usajili wa hukumu hiyo ulifutwa na mahakama hiyo kufuatia shauri lililofunguliwa na IPTL na wenzake wakiupinga; lakini benki hizo zikakata rufaa Mahakama ya Rufani kupinga uamuzi huo.

Hata hivyo wajibu rufaa hiyo IPTL, kampuni za Pan African Power Solution (T) Limited (PAP) na VIP Engineering and Marketing Limited wamezibwaga benki hizo baada ya Mahakama ya Rufani kutupilia mbali rufaa hiyo.

Mahakama hiyo katika uamuzi wake ilioutoa Januari 9, 2026 imetupilia mbali rufaa hiyo kufuatia pingamizi la awali lililoibuliwa IPTL na PAP kupitia wakili wao baada ya kukubaliana na sababu moja pekee kati ya tatu za pingamizi hilo.

Hoja hiyo pekee iliyotosha kumaliza rufaa hiyo ni warufani, Benki za Standard kushindwa kuwatumia wajibu rufaa, IPTL, PAP na VIP, nakala ya hati ya rufaa hiyo kinyume na matakwa ya kanuni ya 97(1) ya Kanuni za Mahakama ya Rufaa.

Rufaa hiyo namba 386 mwaka 2022 ilisikilizwa na jopo la majaji watatu, Dk Mary Levira (kiongozi wa jopo), Leila Mgonya na  Gerson Mdemu.

Katika hoja hiyo, wakili wa IPTL na PAP, Musa Mhagama alidai kuwa mjibu rufaa wa kwanza na wa pili, IPTL na PAP hawakuwahi kupokea nakala ya hati ya rufaa (sababu za rufaa), licha ya kutoa anuani yao ya kupokelea nyaraka.

Hivyo, wakili Mhagama aliiomba mahakama kuitupilia mbali rufaa hiyo kwa madai kuwa haikidhi matakwa ya Kanuni ya 97(1) ya Kanuni za Mahakama ya Rufaa ya Tanzania.

Wakili wa warufani, Gaspar Nyika akijibu hoja hiyo alidai kwamba kumbukumbu ya rufaa (vitabu vya nyaraka za rufaa) ilitumwa kwa mawakili Charles Shipande, Alex  Balomi na Omary Omary, kutoka Legal Clinic Advocates, kupitia wakili Omary aliyejitokeza mahakamani.

Hivyo alidai kuwa hakukuwa na ukiukwaji wa Kanuni ya 97(1) ya Kanuni za Mahakama ya Rufani na akaiomba pingamizi hilo litupiliwe mbali.

Hata hivyo wakili Mhagama alisisitiza kuwa wateja hawakutumiwa nyaraka hiyo na kwamba, mawakili waliotumiwa walikuwa wa Legal Clinic Advocates ambao hawakuwa na maagizo ya kuwawakilisha, akibainisha kuwa walipokea nyaraka hizo kwa Msajili wa Mahakama ya Rufaa.

Mahakama katika uamuzi wake imesema kuwa kuwa kimsingi, utumaji wa hati ya rufaa kwa mjibu rufaa ni takwa la lazimkwa kwa mujibu wa Kanuni ya 97(1) ya Kanuni.

Kwa mujibu wa amri ya mahakama iliyosainiwa na Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufaa, Wanja Hamza, majaji walikubaliana kuwa rufaa hiyo ilikuwa na kasoro za kisheria na hivyo haikuwa na msingi wa kuendelea kusikilizwa.

IPTL, Pan Africa Power Solutions (T) Limited na VIP Engineering and Marketing Limited, waliotajwa kama wadaiwa, waliwasilisha pingamizi tatu za awali. Walidai kuwa walalamikaji walishindwa kuwasilisha Hati ya Rufaa kwa wadaiwa kinyume na Kanuni ya 97(1) ya Kanuni za Mahakama ya Rufaa, waliwasilisha rufaa hiyo nje ya muda uliowekwa kinyume na Kanuni ya 90(1), na pia walikuwa wakifuatilia madai ambayo tayari yalishatatuliwa.

Aidha, wadaiwa waliiambia mahakama kuwa amri (decree) iliyotolewa na Mahakama Kuu katika Shauri la Madai Na. 90 ya 2018 iliifanya mahakama kuwa functus officio, hivyo kuondoa msingi wowote wa kuendelea na shauri hilo.

Akizungumzia uamuzi huo, Mwenyekiti Mtendaji wa IPTL, Harbinder Singh Sethi, aliishukuru mahakama kusimamia haki na kutupilia mbali rufaa hiyo.

“Tunaishukuru Mahakama ya Rufaa kwa kusimamia haki na kutupilia mbali rufaa isiyo na sifa,” alisema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *