Vikosi vya Somalia, Uganda na Umoja wa Afrika (AU) jana Alhamisi viliwaangamiza zaidi ya wanamgambo 30 wa al-Shabaab, na kujeruhi wengine kadhaa wakati wa operesheni ya pamoja huko kusini mwa Somalia.

Operesheni hiyo ilifanywa kwa usaidizi wa washirika wa kimataifa, ikijumuisha mashambulizi ya anga na ardhini karibu na kituo cha Bulunagaad cha kuendeshea operesheni dhidi ya maficho ya al-Shabaab, na kudhoofisha uwezo wa uendeshaji wa kundi hilo katika eneo la Lower Shabelle, imesema taarifa ya Kikosi cha Usaidizi na Utulivu cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (AUSSOM).

Taarifa hiyo imeeleza kuwa, operesheni hiyo imejiri baada ya magaidi wa al-Shabaab kushambulia jeshi la Somalia na askari wa AUSSOM waliokuwa wanawasaka wapiganaji hao, ambao walikuwa wamefurushwa kutoka miji iliyoko kando ya pwani wakati wa ‘Operesheni ya Upanga Uliofichwa’ inayoongozwa na Jeshi la Somalia.

Kikosi cha Usaidizi na Utulivu cha Umoja wa Afrika nchini Somalia kimesema kwamba, vikosi waitifaki vitaendelea na juhudi za kudhoofisha uwezo wa al-Shabaab na kurejesha amani ya kudumu, utulivu, na usalama katika eneo zima la Pembe ya Afrika.

Haya yanajiri siku moja baada ya Wizara ya Ulinzi wa Somalia kusema kwamba, Jeshi la Kitaifa la nchi hiyo limewaua magaidi 17 wa al-Shabaab katika operesheni ya anga iliiyofanyika katika eneo la Jabad Godone katika jimbo la Shabelle ya Kati, kusini mwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika. Al-Shabaab imekuwa ikiendesha uasi dhidi ya serikali ya Somalia kwa zaidi ya miaka 16, na mara kwa mara imekuwa ikilenga vikosi vya usalama, maafisa wa serikali, na raia. 

Tangu mwishoni mwa 2024, Jeshi la Kitaifa la Somalia na vikosi vya usalama katika eneo lenye mamlaka ya ndani la Puntland vimeshadidisha mashambulizi ya anga dhidi ya al-Shabaab katika majimbo ya kusini na kati, na dhidi ya ISIS (Daesh) katika eneo la Bari la kaskazini mashariki, kwa ushirikiano na washirika wa usalama wa kimataifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *