Kiwango cha mabadilishano ya biashara kati ya Iran na Afghanistan kinaongezeka. Serikali ya Taliban imetangaza kuwa, uhusiano wa kibiashara kati ya Iran na Afghanistan umeongezeka hadi dola bilioni tatu na nusu.
Akhundzada Abdul Salam Jawad, msemaji wa Wizara ya Viwanda na Biashara ya serikali ya Taliban, ametangaza kwamba, mnamo 2025, kiwango cha uhusiano wa kibiashara wa Iran na Afghanistan kilifikia zaidi ya dola bilioni tatu na nusu, ambapo mauzo ya nje ya Afghanistan kwenda Iran yalikuwa dola milioni hamsini na tatu. Akieleza kuwa, uhusiano wa kibiashara kati ya Iran na Afghanistan unaongezeka, alibainisha kwamba: “Mwaka jana, kiasi cha uagizaji bidhaa wa Afghanistan kutoka Iran kilikuwa dola bilioni tatu na milioni 450. Hivi sasa, Iran inahesabiwa kuwa mshirika mkubwa wa kibiashara wa Afghanistan, na nchi hiyo inaagiza zaidi bidhaa kutoka Iran kuliko nchi jirani na za kikanda.
Chakula, vifaa vya ujenzi (vyuma na saruji), sabuni, mazulia, dawa, bidhaa za usafi, na vifaa vya umeme ni miongoni mwa bidhaa muhimu zaidi zinazosafirishwa kutoka Iran hadi Afghanistan. Kulingana na msemaji wa Wizara ya Viwanda na Biashara ya serikali ya Taliban, ufuta, mbegu za mbogamboga, pamba, matunda yaliyokaushwa, na mawe ya thamani ni vitu muhimu zaidi vinavyosafirishwa kutoka Afghanistan hadi Iran (ASIBUHI)
Maonyesho ya Biashara ya Kimataifa na Fursa za Kiuchumi kati ya Iran na Afghanistan yalifunguliwa mnamo Oktoba 18, 2025, kwa kuhudhuriwa na kundi la maafisa wa Iran na Afghanistan, maafisa wa majimbo, wanaharakati wa kiuchumi, na wakuu wa vyumba vya biashara vya nchi hizo mbili katika Maonyesho ya Kimataifa ya Khorasan Kusini huko Birjand. Maonyesho hayo yalifanyika kwa lengo la kukuza ushirikiano wa kiuchumi, kuimarisha uhusiano wa kibiashara, na kuvutia uwekezaji wa pamoja kati ya Iran na Afghanistan. Zaidi ya makampuni mia moja na vikundi vya kiuchumi kutoka majimbo tofauti ya Iran na wajumbe kadhaa wa biashara kutoka Afghanistan walihudhuria maonyesho hayo, wakionyesha uwezo wao wa hivi karibuni katika nyanja za madini, kilimo, viwanda vya chakula, huduma za kiufundi na uhandisi, na usafiri.

Mkoa wa Khorasan Kusini, ukiwa lango la biashara kati ya Iran na Afghanistan, una jukumu muhimu katika kukuza uhusiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo mbili, na maonyesho haya yalizingatiwa kama hatua madhubuti kuelekea kuongeza maingiliano ya kiuchumi na uwekezaji wa pamoja kati ya sekta binafsi za Iran na Afghanistan.
Pambizoni mwa tukio hilo, kulifanyika vikao vya ushirikiano wa kiuchumi kati ya Iran na Afghanistan huko Birjand, ambapo miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa ni suluhisho za kupanua maingiliano ya mipakani, kuwezesha mauzo ya nje, na kuanzisha muungano wa uwekezaji. Katika mkutano huu wa pamoja, pande hizo mbili zilizingatia uwezo wa biashara wa pande mbili kuwa hadi dola bilioni kumi na kubadilishana mawazo kuhusu uwekezaji wa pamoja katika nyanja za madini, kilimo, vifaa vya ujenzi, na kuanzisha vituo vya kuhifadhia bidhaa nje. Kuongezeka kwa kiwango cha ubadilishanaji wa biashara kati ya Iran na Afghanistan mwaka wa 2025 ni matokeo mjumuiko wa mambo ya kiuchumi, kisiasa, na miundombinu ambayo yamesukuma nchi zote mbili kuelekea upande ushirikiano mpana. Kulingana na ripoti rasmi, kiasi cha biashara kati ya nchi hizo mbili mwaka wa 2024 kiliongezeka kwa zaidi ya asilimia themanini na nne ikilinganishwa na mwaka wa kabla yake, na kufikia takriban dola bilioni tatu na milioni kumi na tisa. Mwenendo huu ulieendelea mwaka jana 2025, na ishara nyingi za kuimarisha uhusiano wa kiuchumi zinaweza kuonekana.
Mojawapo ya sababu muhimu zaidi za ongezeko hili ni utegemezi mkubwa wa soko la Afghanistan kwa bidhaa za Iran. Kulingana na ripoti, asilimia 95 ya mauzo ya nje ya majimbo ya mashariki ya Iran yanafanywa Afghanistan, na nchi hiyo inasalia kuwa moja ya maeneo manne makuu ya mauzo ya nje yasiyo ya mafuta ya Iran. Afghanistan ni soko kubwa la bidhaa za Iran kutokana na ukosefu wake wa viwanda vingi na hitaji lake kubwa la bidhaa za msingi, vifaa vya ujenzi, nishati, chakula, na bidhaa za petroli.

Jambo lingine muhimu ni uboreshaji wa njia za usafiri na mipaka. Mnamo 2025, Iran ilitangaza kwamba kiasi cha bidhaa zinazosafirishwa kupitia mpaka wa Dogharun hadi Afghanistan kiliongezeka kwa asilimia 70, na mauzo ya nje kutoka mpaka huo huo pia yaliongezeka kwa asilimia 25. Maendeleo ya barabara, kuongezeka kwa uwezo wa forodha, na taratibu rahisi za kiutawala zimefanya biashara kati ya nchi hizo mbili kuwa nyepesi na ya gharama nafuu.
Zaidi ya hayo, ubadilishaji wa njia za biashara ya Afghanistan kutoka Pakistan hadi Iran umekuwa na jukumu muhimu. Bandari ya Chabahar iliipiku Bandari ya Karachi kwa mara ya kwanza mnamo 2025 na ikawa njia kuu ya biashara ya baharini ya Afghanistan. Ubadilishaji huu wa njia umeongeza utegemezi wa Afghanistan kwa Iran na kwa kawaida umeongeza kiwango cha biashara.
Kwa upande mwingine, mbinu ya serikali ya Taliban ya kupanua uhusiano wa kiuchumi na Iran pia imekuwa na ufanisi katika mchakato huu. Maafisa wa Taliban wam,eeleza mara kadhaa kwamba, wanataka kuvutia uwekezaji wa Iran katika maeneo kama vile migodi, nishati ya jua, na maendeleo ya njia za reli. Mtazamo huu chanya umefungua njia ya kuongezeka mauzo ya nje na ushirikiano wa pamoja.
Hatimaye, sifa za bei za bidhaa za Iran ikilinganishwa na washindani kama vile Uturuki, Pakistan, na Asia ya Kati zimesababisha soko la Afghanistan kuendelea kuvutiwa na Iran. Ukaribu wa kijiografia, kufanana kiutamaduni, na gharama za chini za usafirishaji pia ni mambo yaliyoimarisha na kuongeza sifa hii.
Jumla ya mambo haya yanaonyesha kwamba, ongezeko la biashara kati ya Iran na Afghanistan mwaka wa 2025 si mwenendo wa muda mfupi, bali ni matokeo ya mfululizo wa mabadiliko ya kimuundo na mahitaji ya pande zote; muelekeo ambao unaonekana kuwa, utaendelea katika miaka ijayo.