
Miaka 25 baada ya kupitishwa kwa Azimio la Baraza la Usalama namba 1325, lililothibitisha nafasi ya msingi ya wanawake katika ujenzi wa amani, Guterres amesema dunia inaendelea kuwaangusha wanawake na wasichana waliokwama kwenye migogoro — si kwa kukosa nia, bali kwa kukosa hatua na rasilimali.
“Wanawake wajenzi wa amani hawapewi fedha za kutosha, wako hatarini, na hawatambuliwi ipasavyo,” Guterres ameliambia Baraza kwenye mkesha wa kuelekea miaka 25 ya azimio hilo, akisema “na sote tunapoteza – wanawake na wanaume, wasichana na wavulana.”
Mgogoro wa kimataifa wa utekelezaji wa ahadi
Kauli ya Katibu Mkuu imeegemea kwenye takwimu kutoka ripoti yake ya hivi karibuni. Mwaka uliopita, wanawake milioni 676 waliishi ndani ya kilomita 50 kutoka maeneo ya migogoro ya vurugu — idadi kubwa zaidi katika miongo kadhaa.
Matukio ya ubakaji na ukatili wa kingono dhidi ya wasichana viliongezeka kwa asilimia 35, na katika baadhi ya maeneo, wasichana walihesabiwa karibu nusu ya waathirika wote.
Wanawake walioko kwenye nafasi za umma — wanasiasa, waandishi wa habari, na watetezi wa haki za binadamu — wanazidi kulengwa na vitisho na mashambulizi. Vifo vya uzazi vinaongezeka katika maeneo ya migogoro, na wasichana wanakatishwa masomo.
Kujifungua ni changamoto kwa wanawake Gaza
Hoja ya changamoto za wajawazito kwenye mizozo imeungwa mkono na Nourah Erakat, wakili na mwanaharakati mmarekani kwenye asili ya kipalestina ambaye akihutubia Baraza amesema kwa wanawake walioko Ukanda wa Gaza, eneo la Palestina linalokaliwa kimabavu na Israeli, “kiwango cha mimba kuharibika Gaza kimeongezeka kwa asilimia 300. Na hata wanawake wanapoweza kubeba ujauzito hadi mwisho, suala la kujifungua salama ni changamoto.”
Guterres amesema licha ya hali hiyo, taasisi zilizokusudiwa kuwalinda na kuwawezesha wanawake zinakabiliwa na kusambaratika.
Utafiti wa hivi karibuni wa UN Women ulibaini kuwa asilimia 90 ya mashirika ya wanawake ya ndani katika maeneo yenye migogoro yanakabiliwa na matatizo ya kifedha, na karibu nusu yanatarajia kufunga shughuli ndani ya miezi sita kutokana na ukosefu wa fedha.
“Mashirika ya wanawake bado ni njia ya uokozi kwa mamilioni walioko kwenye mizozo,” Guterres amesisitiza. “Lakini yanakosa kabisa rasilimali.”
Kuwekeza kwenye mashirika ya wanawake hakuna mbadala – UN Women
Kwa Sima Bahous, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la masuala ya wanawake, UN Women, “tunaamini hakuna mbadala zaidi ya kubadili mwelekeo huu na kuwekeza kwa kina kwenye mashirika ya wanawake yaliyoko kwenye maeneo yenye mizozo.”
Hata hivyo amekumbusha kuwa, “ingawa ajenda ya wanawake, amani na usalama imepewa kipaumbele katika miji mikuu ya dunia na miji mikubwa ya nchi zilizokumbwa na migogoro, ni lazima pia iendelezwe katika ngazi za jamii na kufika maeneo ya ndani zaidi yanayoathiriwa vibaya — ambako inaweza kuleta mabadiliko makubwa zaidi.”
Kutoka maneno hadi matokeo
Ingawa zaidi ya mataifa 100 yamepitisha mipango ya kitaifa ya utekelezaji wa ajenda ya Wanawake, Amani na Usalama (WPS), utekelezaji wake bado ni wa kusuasua. Kumekuwa na mafanikio fulani, kama kuongeza ushiriki wa wanawake katika operesheni za ulinzi wa amani na kujumuisha vipengele vya kijinsia katika makubaliano ya amani.
Hata hivyo, Guterres ameonya kuwa mafanikio hayo ni dhaifu na yanarudi nyuma, hasa kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya kijeshi na mashambulizi ya tawala za kimabavu dhidi ya haki za wanawake.
Ametoa wito kwa serikali, wafadhili na mashirika ya kimataifa kuacha maneno matupu na kuleta mabadiliko yanayopimika.
“Dunia haitaki kukumbushwa zaidi kuhusu ukweli huu,” amesema. “Inahitaji kuona matokeo yanayoakisi ukweli huo.”
Nini kifanyike?
Guterres ametoa mwelekeo wa kufufua ajenda ya WPS na kurejesha kasi ya maendeleo:
- Ufadhili: Kupatia kipaumbele kwa kuongezeka kwa msaada wa kifedha wa moja kwa moja, rahisi na wa ubora kwa mashirika ya wanawake, hasa katika maeneo ya migogoro.
- Ushiriki: Kuhakikisha ushiriki kamili, sawa na wenye maana wa wanawake katika michakato ya amani kupitia viwango vya lazima na nafasi maalum.
- Uwajibikaji: Wahusika wa ukatili wa kijinsia na kingono unaohusiana na migogoro wawajibishwe.
- Ulinzi: Kutekeleza sera ya kutovumilia kabisa ukatili dhidi ya wanawake wajenzi wa amani na watetezi wa haki za binadamu.
- Ujumuishaji wa sera:Kujumuisha na kuingiza misingi ya WPS katika sheria, mipango, bajeti na taasisi za kitaifa.
- Usalama wa kiuchumi: Kuwekeza katika haki za kiuchumi za wanawake, ikiwemo ajira na ulinzi wa kijamii.
- Takwimu za kijinsia: Kuanzisha “mapinduzi ya takwimu za kijinsia” ili kujaza pengo la taarifa, hasa kuhusu ukatili wa kingono kwenye migogoro.