
UNESCO ni shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni ambalo kupitia maadhimisho ya siku ya walimu duniani Oktoba 5, ilitangaza kaulimbiu kuwa ni Kubadilisha ualimu kuwa taaluma ya ushirikiano, ikisisitiza uwezo wa kubadilisha hali kupitia ushirikiano kwa walimu, shule na mifumo ya elimu.
Bwana Vargas kupitia mahojiano yaliyochapishwa kwenye chaneli ya YouTube ya UNESCO katika kuthibitisha umuhimu wa kushirikisha walimu akarejelea utafiti uliofanyika katika nchi 19 za Amerika Kusini na Karibea kuhusu matokeo ya kujifunza.
Utafiti ulibaini kwamba “shule zilizofanya vizuri zaidi zilikuwa zile ambazo uongozi wa shule ulikuwa shirikishi, ukishauriana na walimu ambao walikuwa wakishirikiana na jamii. Kwa hiyo mwisho wa siku, mtu anagundua kwamba uongozi mzuri wa shule una matokeo, si tu katika hali ya mazingira ya shule na ustawi wa walimu, bali pia katika matokeo bora ya kujifunza kwa wanafunzi. Hiyo ndiyo aina ya kazi ambayo viongozi wa shule wanaweza kufanya.”
Na alipoulizwa iwapo Akili Mnemba au Unde itaondoa nafasi ya mwalimu, Bwana Vargas amesema, “nadhani akili unde, kama tunavyoanza kuona, ina uwezo wa kupunguza mzigo wa kazi wa walimu ili waweze kujitolea kikamilifu kwenye kipimo hiki cha uhusiano na hisia katika kujifunza, ambacho tunajua ni muhimu sana. Lakini jinsi ya kushirikisha wanafunzi, jinsi ya kuwasaidia kufikiria kazi watakayopenda kufanya baadaye, jinsi ya kufundisha kulingana na mahitaji ya mwanafunzi, ningesema, ni jukumu ambalo walimu watabakia nalo.”