Historia muda wote imethibitisha kwamba, msimamo imara na kutotetereka mataifa ya dunia katika kupigania ukombozi, siku zote hushinda utumiaji mabavu, vita, njama na mauaji ya umati. Hiyo ni ahadi ya Qur’ani Tukufu ambapo katika Surat Muhammad, aya ya 7 tunasoma: “Mkimnusuru Mwenyezi Mungu basi na Yeye atakunusuruni.”

Tarehe 7 Oktoba 2023, Operesheni yenye kuleta ghera na fakhari ya Kimbunga cha al-Aqsa iliendeshwa na wanamapambano wa Palestina wakiongozwa na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS na kutoa pigo kubwa mno la kihistoria kwa utawala wa Kizayuni wa Israel. Operesheni hiyo ya kishujaa na ya ya kushtukiza ilikuwa jibu la lazima la miongo kadhaa ya uvamizi wa kijeshi, kuzingirwa Ukanda wa Ghaza na jinai za kibinadamu zinazofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina. 

Operesheni ya kimbunga cha al-Aqsa ilifanyika katika eneo la mpaka kati ya Ghaza na ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu ambazo zimepachikwa jina bandia la Israel. Operesheni hiyo ilianza wakati wa alfajiri. Vikosi vya Hamas kwanza walipiga maeneo ya Wazayuni kwa kutumia maroketi na walirusha makombora 5,000. Baada ya hapo, walivuka ukuta uliojengwa na jeshi la Israel na kuingia kwenye maeneo ya walowezi wa Kizayuni. Taarifa zinasema kuwa, zaidi ya wanajeshi 1,400 wa Israel waliangamizwa na 3,500 wengine walijeruhiwa kwenye operesheni hiyo ya kishujaa.

Wanamapambano wa Hamas waliongoza operesheni kwa ufanisi wa hali ya juu kiasi kwamba hata walifanikiwa kukamata kundi la wanajeshi wa Kizayuni na kuwahamishia Ghaza kama ngawira. Operesheni hiyo ilikuwa ni pigo kubwa mno kwa Israel kwa namna ambayo haijawahi kutokea katika historia yake yote. Amri ya operesheni hiyo ilitolewa na “Mohammed Deif”, mmoja wa makamanda wa Brigedi za Izzuddin al Qassam, Tawi la Kijeshi la HAMAS. Duru za kuaminika zinasema kuwa, Mohammed Deif na Yahya Sinwar, makamanda wawili wa Hamas ambao walikuwa wamefungwa katika magereza ya Israel kwa miaka mingi, ndio waliobuni na kusimamia uendeshaji wa operesheni ya kifakhari ya “Kimbunga cha Al-Aqsa.”

Kimbunga cha Al-Aqsa lilikuwa ni jibu lisiloepukika la Wapalestina kwa jinai za utawala wa Kizayuni unaoyakalia kwa mabavu maeneo ya Wapalestina. Hilo lilikuwa ni jibu la jinai ya kuugeuza Ukanda wa Ghaza kuwa gereza kubwa zaidi la wazi duniani kwa zaidi ya miaka kumi na sita na kuwanyima wakaazi wake haki za kimsingi zaidi za kuishi.

Ayatullah Khamenei, Kiongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema hivi kuhusu Operesheni ya Kimbunga cha al Aqsa: “Pigo hilo wamelitaka wenyewe kwa vitdondo vyao wenyewe hao Wazayuni. Wakati ukatili na jinai za Wazayuni zilipovuka kikomo na wakati unyama wao ulipofikia kileleni, kila mtu angetarajia kutoikea operesheni kama hiyo…”

******

Katika kukabiliana na Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa, utawala huo ghasibu wa Israel unaendelea hadi hivi sasa kufanya jinai za kivita na maafa makubwa ya kibinadamu. Utawala huo unaochikiza sana duniani umefanya mauaji makubwa zaidi ya umati katika karne ya 21. Imekuwa ikifanya mashambulizi ya kikatili mno dhidi ya wananchi wa Ghaza kwa miaka miwili sasa. Mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel na hatua ambayo lengo lake kuu ni kuangamiza kabisa jamii ya Wapalestina na hilo ndilo lengo kuu la miaka yote hii la utawala wa Kizayuni. 

Tangu saa za kwanza kabisa za baada ya Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa, Israel ilionesha kwamba ilikuwa imeamua kutoheshimu sheria na kanuni yoyote ya vita. Iliamua kuonesha chuki na uadui wake dhidi ya miundombinu, majengo ya makazi ya watu, mauaji ya raia, wanawake na watoto, kuripua vituo vya matibabu, mahospitali, kuua madaktari, kushambulia maeneo ya misaada ya Umoja wa Mataifa kushambulia maskuli kutumia silaha zilizopigwa marufuku na jinai nyinginezo nyingi kwa kisingizio cha eti kukabiliana na Hamas. Uhalifu wote wa Israel huko Ghaza katika kipindi cha miaka miwili hii umesababisha majanga ya kibinadamu ambayo yote yametokea kutokana na kimya cha Umoja wa Mataifa, taasisi zinazodai kupigania haki za binadamu duniani na wanasiasa Wazayuni wenye mfungamano na Marekani na Israel.

Kwa kuharibu kwa makusudi maelfu ya makazi, Wazayuni walifanya kwanza mamilioni ya watu kukosa makazi na kuwaweka kwenye hatari za mazingira na usalama. Takwimu zinaonesha kuwa ukubwa wa uharibifu wa majengo ya makazi ya watu katika miaka miwili iliyopita hauaminiki. Ni watoto wangapi wasio na hatia walioachwa chini ya vifusi na ni wanawake wangapi walizikwa na watoto wao chini ya vifusi?

Israel pia imeharibu miundombinu ya mijini huko Ghaza, na kuifanya Ghaza kutoka eneo linalokaliwa na watu kuwa jehanamu isiyowezekana kuvumilika. Kukatwa kabisa na mfululizo umeme na mafuta, hata kwa hospitali na mitambo ya matibabu, kumeweka wakaazi wengi, haswa wagonjwa, katika shida. Kwa kukatika umeme, watoto wachanga kwenye mashine za oksijeni katika hospitali wamekuwa wahanga wadogo zaidi wa wanaokandamizwa, wakifa mmoja baada ya mwingine. Vitendo hivi vya kinyama ni kielelezo tosha cha matumizi ya kunyimwa haki ya msingi kama silaha ya vita, jambo ambalo ni kinyume na sheria zote za kimataifa.

Mashirika ya kimataifa, ambayo yameamua kukaa kimya na kutosheka tu na kutaja takwimu za maafa ya jinai wanazofanyiwa Wapalestina, yamekiri kwamba idadi ya watoto waliouawa huko Ghaza katika wiki chache tu za kuanza jinai za Isrfael ilikuwa kubwa kuliko idadi ya watoto wote waliouawa katika kipindi cha mwaka mzima wa kwanza wa vita vikuu vya dunia. Mauaji hayo ya kikatili na ya makusudi yalilenga kuonesha kuwa, maisha ya Wapalestina hayana thamani yoyote mbele ya wavamizi.

Hospitali, skulina vituo vya misaada vya Umoja wa Mataifa, kama vile vituo vya UNRWA, pia vimekuwa vikishambuliwa mara kwa mara kwenye mashambulizi ya anga na ya ardhini katika miaka hii miwili ya jinai za Israel. Kushambuliwa hospitali kama vile “Al-Shifa” na “Al-Quds” wakati wagonjwa, majeruhi na waliohamishiwa kwenye hospitali hizo, hakukufanyika kimakosa, bali zilikuwa ni jinai za kitaasisi za kujaribu kuwalazimisha Wapalestina kuhama Ukanda wa Ghaza. Kushambuliwa kwa makombora mahema ya wakimbizi wa Ghaza na hata kuripuliwa kwa makusudi makao ya waandishi wa habari ni miongoni mwa jinai chafu za utawala wa Kizayuni kwenye mashambulizi yake hayo.

Kushambuliwa kwa makusudi Misikiti na makanisa, bila ya kujali kwamba hayo ni maeneo ya kihistoria ya ya kidini kwa Palestina na duniani kwa ujumla, pia kulifanywa na Israel ili kuonesha kwamba baada ya kumalizika mashambulizi yake huko Ghaza, hakutakuwa kumebakia nembo yoyote ya kidini, kihistoria na kiutamaduni ya Wapalestina. 

Jinai za Israel huko Ghaza baada ya kimbunga cha Al-Aqsa imefanikiwa kuondoa kizoro kwenye uso wa ulaghai na udanganyifu kaktika uso uliojaa uchafu wa utawala wa Kizayuni na zimefichua sura yake halisi ya kikatili na umwagaji damu. Sasa, viongozi Israel wanaosakwa kimataifa kwa kutenda jinai za kutisha, wameamua kufanya mauaji ya umati wazi wazi kwa kutumia njaa, kiu na kuwanyima haki watu wanaodhulumiwa wa Ghaza, jambo ambalo ni ukiukaji wa wazi wa Mikataba ya Geneva.

Kitendo cha Israel cha kufunga kabisa mipaka na kuzuia kuingizwa vitu muhimu kama vile dawa, chakula na mafuta huko Ghaza, si tu kimewaweka wakazi wa ukanda huo chini ya mzingiro mkali zaidi wa kijeshi, lakini pia inawasababishia wananchi wasio na hatia wa Ghaza vipo vya polepole hasa wanawake na watoto wadogo malaika wa Mungu wasio na kosa lolote. Utawala huo katili hauna huruma hata kwa watoto wadogo, wanawake na wanaume wanaotembea kilometa nyingi kutafuta chakula cha angalau kunyamazisha vilio vya watoto wao wachanga. Wapalestina wengi wanauliwa kikatili na wanajeshi makatili wa Kizayuni wakati wanapokusanyika kusubiri chakula kwenye maeneo ambayo ni Israel na Wamarekani wenyewe ndio waliyoyaainisha na kudai ni maeneo salama. Kinachosikitisha zaidi ni ukimya wa jamii ya kimataifa ambayo haichukui hatua yoyote ya kuulazimisha utawala wa Kizayuni kukomesha jinai na ukatili wake huo ambao haujawahi kushuhudiwa katika historia. 

Kwa hakika, moja ya matukio machungu zaidi ya mauaji hayo ya umati ni kimya hicho cha aibu cha jamii ya kimataifa wakati muda wote mashirika yanayodaiwa ni ya kimataifa, hayaoni hata soni kujitokeza hadharani na kujinadi kuwa eti yanatetea haki za binadamu. Serikali za nchi za Magharibi, hususan Marekani na washirika wake wa Ulaya zinaunga mkono waziwazi jinai za Israel. Haziungi mkono kwa maneno na kisiasa tu, bali pia zinausheheneza utawala wa Kizayuni silaha kali za kufanyia mauaji ya umati huko Ghaza.

Kwa kutuma mabomu, risasi na zana za kijeshi kwa Israel, Marekani ndiyo inayoongozwa katika kuusheheneza utawala katili wa Israel mavomu, risasi na silaha kali za kijeshi. Marekani ndiye mshirika nambari moja wa mauaji ya kimbari huko Ghaza. Kwa kweli msaada mkubwa wa kijeshi wa nchi za Magharibi kwa utawala wa Kizayuni unaofanya mauaji ya kutisha dhidi ya watoto wadogo, ni ushahidi wa kutosha wa unafiki mkubwa unaoudhibiti mfumo wa kimataifa duniani leo.

Wakati huo huo, vyombo vya habari vya Magharibi vinavyojaribu kwa njia zote kuhalalalisha jinai Israel kamwe havitumii neno mauaji ya umati vinapotangaza habari za jinai za Israel bali vinadau tu eti mauaji ya Ghaza. Kikubwa kinachoakisiwa na vyombo hivyo vya habari vya Magharibi ni kuhakikisha muda wote vinapandikisha madai ya uongo ya eti Israel inajihami. Lakini propaganda zote hizo zimeshindwa kuzuia mwamko wa walimwengu kuhusu uhakika wa kijinai wa Israel. Damu ya watoto wa Palestina imeyaamsha mataifa ya dunia, na ndio maana maandamano ya maelfu kwa maelfu ya wapenda haki duniani yanafanyika mara kwa mara kwenye mataifa tofauti hasa ya Ulaya na Magharibi kuwaunga mkono watu wasio na hatia wa Ghaza na kudhihirisha ukubwa wa hasira za walimwengu mbele ya jinai za Israel.

Baada ya kufanyika kwa mafanikio Operesheni ya Kimbunga cha al Aqsa, utawala pandikizi wa Kizayuni haukutosheka tu na kuishambulia kwa mabomu Ghaza, bali umeua pia viongozi waandamizi wa kambi ya Muqawama ndani na nje ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni. Kwa huko Ghaza utawala wa Kizayuni umewaua shahidi makamanda wa HAMAS, Yahya Sinwar, na Muhammad Abu Dheef na kabla yake ulimuua shahidi Ismael Haniyeh, mkuu wa harakati ya HAMAS. Hawakuishia hapo, bali waliwaua shahidi pia viongozi wengine wa Muqawama kama Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon, Sayyid Hassan Nasrullah na maafisa wengine wakuu wa Hizbullah huko Lebanon. Utawala huu pia ulishambulia Iran ya Kiislamu na kuua makamanda wakuu wa kijeshi na wasomi wa kisayansi wa Iran. Lakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitoa jibu kali kwa Israel mtenda jinai katika vita vya siku 12 na kuharibu miundombinu yake muhimu sana. Makombora ya Iran ya masafa marefu na yanayoongozwa kwa usahihi yaliiaibisha mifuno ya kujilinda kwa makombora ya madola ya Magharibi ukiwemo mfumo wa Iron Dome wa Israel na kuigeuza kuwa kichekesho mbele ya vyombo vya habari Duniani! Kipigo kikali kilichotolewa na Iran ya Kiislamu kwa Israel lilikuwa ni tangazo la wazi kwamba Iran bado iko imara kwenye kambi ya Muqawama. Kuunga mkono Muqawama wa Palestina ni moja ya sera zisizobadilika za Iran ya Kiislamu, na uungaji mkono huu utaendelea hadi ukombozi kamili wa Palestina na Quds Tukufu ambayo ina Msikiti wa al Aqsa ambao ni Kibla cha Kwanza cha Waislamu.

Si tu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitoa jibu kali la kijeshi kwa Israel, bali pia hadi hivi sasa inapambana kukomesha mauaji ya kimbari na jinai za kivita zinazofanywa na Israel. Iran inanedesha mapambano makubwa ya kimataifa kwa ya kidiplomasia ili kukomesha jinai za Israel kwenye Ukanda wa Ghaza. Jamhuri ya Kiislamu inapigania mno kuhakikisha kwamba viongozi wa utawala ghasibu wa Israel wanaoua watoto kijinai na kinyume cha sheria, waburuzwe mahakamani na kuadhibiwa moja kwa moja katika mahakama za kimataifa ikiwemo Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC).

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina imani kwamba kipindi hiki cha giza kitaisha na ushindi utakuwa wa Wapalestina kwa kusimama imara vikosi vya Muqawama na maandamano ya kimataifa dhidi ya jinai za Israel. Historia inaonesha kwamba mapenzi ya mataifa ya uhuru yatashinda vita na njama za mauaji ya umati, na bila ya shaka yoyote ahadi ya Quran itatimia kama tulivyonukuu mwanzoni mwa kipindi hiki aya ya 7 ya Surat Muhammad ya Qur’ani Tukufu inayosema: “Mkimnusuru Mwenyezi Mungu basi na Yeye atakunusuruni, ambapo moja ya tafsiri za aya hiyo ni ile inayosema: “Mkipigana katika njia ya Mwenyezi Mungu kwa dhati bila ya shaka Mwenyezi Mungu atakunusuruni.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *