Macron amempa Lecornu jukumu la kuendesha mazungumzo na vyama vya siasa ili kutafuta njia za kurejesha utulivu wa kisiasa. Hatua inayopingwa vikali na upinzani na hata washirika wa Macron wakiwemo mawaziri wa zamani wakisema kuwa uchaguzi wa mapema wa rais ndiyo suluhisho sahihi la mkwamo wa kisiasa nchini humo.
Lecornu, ambaye alikuwa waziri mkuu wa tatu kushika wadhifa huo tangu kufanyika kwa uchaguzi wa ghafla wa bunge mwaka jana, alitangaza kujiuzulu baada ya serikali yake kukataliwa na pande zote — wapinzani na hata baadhi ya washirika wa Macron. Serikali hiyo ilikuwa ya muda mfupi zaidi katika historia ya kisasa ya Ufaransa.
Baada ya kujiuzulu, Rais Macron amempa Lecornu jukumu jipya la kufanya mazungumzo ya siku mbili na vyama mbalimbali vya siasa kwa lengo la kutafuta mwafaka wa kisiasa. Hata hivyo, hatua hiyo imeonekana na wengi kama njia ya kujiongezea muda, badala ya kutafuta suluhisho la kweli.
Upinzani wapendekeza mwelekeo tofauti
Wanasiasa mashuhuri akiwemo waziri mkuu wa zamani, Edouard Philippe, pamoja na kiongozi wa chama cha mrengo wa kulia, Jordan Bardella, wametaka uandaliwe uchaguzi wa rais wa mapema ili kutatua mkwamo uliopo. Wanahoji kuwa mfumo wa sasa wa bunge usio na wingi wowote wa wazi, unataka kufanyike maamuzi makubwa ili kuirejesha Ufaransa katika muelekeo wa utulivu wa kisiasa.
Waziri mkuu wa zamani wa Ufaransa Gabriel Attal amesema: “Sielewi tena maamuzi haya. Tangu kuvunjwa kwa serikali, jambo ambalo lenyewe halieleweki, maamuzi mengi yamekuwa yakitoa hisia kwamba hakuna nia ya kushirikiana katika madaraka, ilhali kila kitu katika matokeo haya kinaelekeza tushirikiane.”
Hatma ya serikali ni ipi?
Kwa sasa, swali linaloulizwa ni je, Macron atafanya nini? Muda uanzidi kuyoyoma, kwani anapaswa kuondoka madarakani ifikapo 2027 baada ya kutumikia mihula miwili ya urais, wataalamu wa siasa wanajadili uwezekano wa hoja kadhaa. Hata hivyo, hakuna hata moja inayotoa suluhisho la haraka.
Inaonekana Macron anajitengenezea njia ya kumteua tena Lecornu, badala ya Bruno Le Maire, waziri wa zamani wa fedha ambaye uteuzi wake kama waziri wa ulinzi ulisababisha mgogoro huu, kusema atajiondoa serikalini.
Lakini haijulikani ikiwa Lecornu ataweza kuunda serikali — au kama hata kufanikiwa katika kura ya imani bungeni, ambako serikali yake haina wingi.
Hatua nyengine ni iwapo Macron atamteua waziri mkuu mwingine mpya, huyo atakuwa waziri mkuu wa nane katika kipindi cha utawala wake na wa tatu mwaka huu pekee — jambo lisiloonekana vyema kwa taswira ya kisiasa ya Ufaransa.
Macron amekuwa akikataa mara kwa mara wito wa kuitisha uchaguzi wa mapema wa bunge, hasa baada ya hatua yake ya awali ya kuitisha uchaguzi wa haraka majira ya joto 2024 kumgeukia na kumwacha na bunge lililogawanyika.