Akizungumza kwa niaba ya PostaMasta Mkuu, Mkurugenzi wa Huduma za Posta Arubee Ngaruka amemweleza Sabrina Said wa Idhaa ya Umoja wa Mataifa huko Dar es salaam,Tanzania kwamba wanakwenda sambamba na mabadiliko na maendeleo ya kidijitali ili kuhakikisha wanamfikia kila mtu kokote aliko.
Arubee Ngaruka (kushoto), Mkurugenzi wa huduma za Posta, Shirika la Posta Tanzania, akizungumza na Sabrina Moshi wa UN News Kiswahili
Posta kiganjani
Kauli yake inaendana na kaulimbiu ya siku ya posta duniani mwaka huu ambayo ni “Posta kwa ajili ya Watu: Huduma za Kijamii. Ufikaji wa Kimataifa”
Bwana Ngaruka amesema, “unafahamu sasa hivi dunia inakwenda kasi, dunia na kimbia sana na teknolojia. Na sisi Shirika la Posta tuko chini ya Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari. Na Katika eneo la teknolojia tunahakikisha tunaenda nayo kama dunia inavyotaka kwenda.”
Amesema kwamba , “tumejaribu kuhakikisha kwamba sasa hivi huduma zetu zote zimeingia ziko kwenye kidigitali zaidi. Ukiangalia tuna apu yetu ili huduma ya posta iweko kiganjani. Ukipakua apu kwenye Playstore au sehemu nyingine utaikuta ipo na huduma zimo.”
Ni kwa kupitia teknolojia ya kiganjani, mteja anaweza sasa kufuatilia barua au kifurushi chake baada ya kutuma kwa njia ya posta. Halikadhalika iwapo hawezi kufika ofisi ya posta, mtumishi wa posta anaweza kufika kwenye makazi yake kuchukua mzigo au barua husika.
Guterres ashukuru wafanyakazi wa posta
Katika ujumbe wake wa siku hii, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amewashukuru wafanyakazi milioni 4.6 wa posta wanaounganisha jamii kote duniani.
Guterres amesema, “Posta ni huduma inayotolewa na watu, kwa watu. Leo na kila siku, tunawashukuru wafanyakazi wa posta na kuahidi kuunga mkono huduma thabiti na endelevu ya posta kwa jamii na kwa dunia yetu”.
Amesisitiza jukumu muhimu la mitandao ya posta katika utumaji sio tu wa barua, bali pia huduma muhimu, fursa, na kuaminiana kuunganisha vijiji na miji, kuondoa pengo kati ya vijijini na mijini, na kufanya dunia iweze kufikiwa na kila mtu.