
Dar es Salaam. Zaidi ya wanawake 200 wanaojishughulisha na utengenezaji wa bidhaa za batiki wamenufaika na mafunzo ya usalama na afya mahali pa kazi yaliyotolewa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA).
Mafunzo hayo ya siku moja yaliyoandaliwa na OSHA yamefanyika Dar es Salaam yakilenga kuwajengea uwezo wajasiriamali hao katika kutekeleza shughuli zao za uzalishaji kwa kuzingatia kanuni za usalama na afya.
Washiriki walijifunza mada mbalimbali ikiwemo dhana ya usalama na afya kazini, utambuzi wa vihatarishi katika uzalishaji wa batiki, na huduma ya kwanza mahali pa kazi.
Akifungua mafunzo hayo, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano ya Kazi), Rahma Kisuo, amesema serikali inaendelea kuimarisha usalama na afya kwa makundi ya wajasiriamali wadogo kutokana na mchango wao mkubwa katika ukuaji wa uchumi.
“Wajasiriamali wadogo ni nguzo muhimu katika ujenzi wa uchumi wa Taifa. Ni lazima tuwahakikishie mazingira salama ili waweze kufanya kazi zao bila kuhatarisha afya na maisha,” amesema.
Amesema mafunzo hayo yatasaidia kupunguza ajali, magonjwa na vifo vinavyotokana na ukosefu wa mifumo bora ya usalama na afya, na akaitaka OSHA kuhakikisha elimu hiyo inatolewa kwa mtiririko endelevu kwa makundi mbalimbali nchini.
Aidha, amewataka wajasiriamali hao kuepuka makundi yenye nia ya kuchochea vurugu na kuhatarisha amani ya nchi.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, amesema mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa programu ya Afya Yangu, Mtaji Wangu inayolenga kupunguza utofauti wa uelewa kuhusu masuala ya usalama na afya baina ya sekta rasmi na ile isiyo rasmi.
“Kupitia programu hii tumekuwa tukiainisha makundi ya wajasiriamali wadogo, kuwapa mafunzo na kuwapatia vifaa kinga kulingana na aina ya shughuli zao,” amesema Mwenda.
Ameongeza kuwa tathmini za OSHA zimebainisha kuwa vijana ndio waathirika wakubwa wa ajali kazini kutokana na uelewa mdogo na kukosa uzoefu, hivyo programu hiyo itaendelea kuelekezwa zaidi kwao.
Baadhi ya washiriki wameelezea manufaa ya mafunzo hayo, akiwemo Jesca Charles ambaye amesema elimu waliyopata itawasaidia kuboresha usalama katika uzalishaji wa batiki.
“Tumepata vifaa kinga na elimu ya kujikinga dhidi ya kemikali, ambazo ni miongoni mwa vihatarishi vikubwa kwenye kazi zetu. Tunashukuru OSHA kwa kutambua umuhimu wetu,” amesema.