
Makaburi ya Waislamu nchini Australia yamenajisiwa kwa vichwa vya nguruwe vilivyokatwa kufuatia ufyatuaji risasi uliolenga hafla ya Kiyahudi mjini Sydney nchini humo.
Tovuti ya habari ya nchini Australia ya news.com.au imeripoti kuwa video iliyosambazwa jana Jumatatu imeonyesha makaburi ya Waislamu katika kitongoji cha Narellan huko Kusini Magharibi mwa mji wa Sydney yakiwa yamenajisiwa kwa vichwa vya nguruwe na viungo vya mnyama huyo kufuatia tukio la ufyatuaji risasi katika ufukwe wa Bondi huko Sydney.
Polisi ya Australia imeeleza kuwa wamepokea taarifa kuhusu mabaki ya mnyama yaliyoachwa katika lango la kuingia eneo la makaburiya Waislamu katika barabara ya Richardson huko Narellan.
Maafisa polisi walifika katika makaburi hayo na kukuta vichwa kadhaa vya nguruwe. Polisi imeanzsha uchunguzi kuhusu hujuma hiyo. “Vichwa vya nguruwe vimeshaondolewa makaburini na kutupwa ipasavyo,” imesomeka taarifa ya polisi ya Sydney.
Makaburi ya Waislamu katika kitongoji cha Narellan kusini magharibi mwa mji wa Sydney yalinajisiwa jana viungo vya nguruwe siku mbili baada ya polisi ya Australia kutangaza kuwa watu wawili wasiojulikana yaani baba mwenye umri wa miaka 50 na mwanae wa kiume wa miaka 24 walifyatua risasi katika fukwe za Bondi huko Sydney Jumapili jioni na kuuwa Mayahudi 15 na kuwajeruhi wengne 42 ambao walipelekwa hospitali kwa ajili ya matibabu.
Mamlaka za Australia zilisema polisi walimuua kwa risasi mshambuliaji mmoja, huku wa pili akikamatwa na kuripotiwa kuwa katika hali mahututi. Polisi ya Australia imelitaja tukio hilo kuwa la kigaidi.