Tanga. Mradi wa uboreshaji wa barabara ya Tanga-Pangani-Mkange umefikia asilimia 75 ya utekelezaji wake, ikiwa ni hatua muhimu katika uimarishaji wa miundombinu ya usafiri katika ukanda wa Pwani.
Hatua hiyo, imefikiwa mapema wiki hii wakati wa ziara ya Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) mkoani Tanga kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo.
Mhandisi wa mradi huo, Khatibu Ahmad amesema kazi zimefikia asilimia 75 na zinaendelea katika hatua mbalimbali za ujenzi.
Hatua hizo, amesema ni pamoja na usafishaji wa eneo la barabara, uondoaji wa tabaka la udongo usiofaa, uwekaji wa tabaka la kifusi, tabaka la udongo uliochanganywa na saruji na mawe na lami katika baadhi ya maeneo.
Ameeleza hadi sasa mkandarasi amelipwa Sh50.96 bilioni kwa kazi zilizotekelezwa, hatua inayoonesha kasi ya utekelezaji na usimamizi wa karibu wa mradi huo.
Baada ya ukaguzi, bodi hiyo ya Tanroads imeeleza kuridhishwa na hali ya mradi huo unahusisha pia ujenzi wa Daraja la Pangani, ikisisitiza ni miundombinu muhimu inayosaidia kuimarisha muunganiko wa barabara katika ukanda wa Pwani.
Bodi hiyo, imeeleza mradi wa Tanga-Pangani-Mkange ni sehemu ya mkakati wa Serikali kuwekeza katika miundombinu ya kisasa ya usafiri kama nyenzo ya kuchochea maendeleo ya uchumi, kurahisisha huduma za kijamii na kuboresha maisha ya wananchi.
Imeeleza sehemu ya kwanza ya mradi inahusisha uboreshaji wa barabara ya Tanga-Pangani yenye urefu wa kilometa 50, inayoboreshwa kutoka barabara ya changarawe hadi kiwango cha lami.
Uboreshaji huo, bodi hiyo imesema unalenga kuongeza usalama wa watumiaji wa barabara, kupunguza gharama za usafiri na kuboresha mawasiliano kati ya Jiji la Tanga, Wilaya ya Pangani na maeneo ya jirani.
Sehemu ya tatu ya mradi, amesema inahusisha ujenzi wa barabara ya Tungamaa-Mkwaja-Mkange yenye urefu wa kilometa 95.2, ikijumuisha kilomita 3.7 za barabara unganishi ya Kipumbwi.
Bodi hiyo, imeeleza kuwa barabara hiyo ni muhimu katika kuimarisha muunganiko wa maeneo ya Pwani, hususan kwa shughuli za kiuchumi kama uvuvi, kilimo, biashara na utalii.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Mohamed Besta, amesema kazi za ujenzi zinaendelea kwa kasi na matarajio ya wakala huo ni kuona mradi wa Tungamaa-Mkwaja-Mkange unakamilika ndani ya muda uliopangwa.
“Tanroads itaendelea kumsimamia kwa karibu mkandarasi na mhandisi mshauri ili kuhakikisha ubora wa kazi na ukamilishaji wa mradi kwa wakati,” amesema.
Amesema matarajio ya Tanroads ni kuona ifikapo katikati ya mwaka ujao mradi huo unakuwa umekamilika, jambo litakalowanufaisha wananchi na kuimarisha usafiri katika barabara inayounganisha Tanzania na Kenya kupitia mtandao wa barabara za Jumuiya ya Afrika Mashariki unaofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).
Mradi huo unafadhiliwa kwa pamoja na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo hadi sasa mkandarasi amelipwa jumla ya Sh52 bilioni.
Barabara hiyo ni sehemu ya ushoroba muhimu wa Pwani unaounganisha Malindi nchini Kenya kupitia Lungalunga, Hororo, Tanga, Pangani hadi Bagamoyo na Dar es Salaam na kukamilika kwake kutaimarisha muunganiko wa bandari za Mombasa, Tanga na Dar es Salaam. Hivyo kuongeza ushindani na ufanisi wa biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki.