Takribani waandishi wa habari 14 walikamatwa nchini Venezuela siku ya Jumatatu walipokuwa wakiripoti kuhusu mgogoro uliosababishwa na operesheni ya kijeshi ya Marekani iliyomkamata kiongozi wa nchi hiyo, Nicolás Maduro.
Muungano wa wafanyakazi wa vyombo vya habari nchini humo ulieleza kuwa karibu wote waliokamatwa, isipokuwa mmoja, walikuwa wakifanya kazi kwa mashirika ya habari ya kimataifa.
Wengi wao waliachiliwa huru baadaye siku hiyo, huku mwandishi mmoja akifukuzwa nje ya nchi.
Vyombo vya habari vya kigeni kwa muda mrefu vimekuwa vikikabiliwa na vikwazo vikali nchini Venezuela, na ni idadi ndogo tu ya waandishi wa habari wanaopata viza za kufanya kazi nchini humo.
Kukamatwa kwa waandishi hao kulijiri wakati Delcy Rodríguez aliapishwa kuwa rais wa mpito, muda mfupi baada ya kutangaza kuwa yuko tayari kushirikiana na utawala wa Rais Donald Trump, ambao alidai ungekuwa na nafasi ya kuisimamia Venezuela.
Kwa mujibu wa muungano huo, waandishi wa habari walikamatwa na vikosi vya usalama katika na pembezoni mwa jengo la Bunge la Taifa, pamoja na katika eneo la Altamira, ndani ya mji mkuu, Caracas.
Angalau wawili walikamatwa na maafisa wa idara ya ujasusi wa kijeshi, huku wengine wakishikiliwa na vyombo vya ujasusi wa kiraia.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa vifaa vyao vilichunguzwa, simu zao zilifanyiwa upekuzi, na jumbe zao za maandishi pamoja na mawasiliano yao ya mitandao ya kijamii zilisomwa bila idhini.
Mwandishi wa habari kutoka Colombia na mwandishi mwingine kutoka Hispania pia walikamatwa katika mpaka wa Venezuela na Colombia, karibu na mji wa Cúcuta.
Matukio hayo yametokea katika kipindi cha mvutano mkubwa wa kisiasa nchini Venezuela, kufuatia kukamatwa kwa Nicolás Maduro na mkewe na vikosi vya Marekani katika uvamizi wa alfajiri uliosababisha vifo vya makumi ya walinzi wake na askari wa usalama.
#KilichoBoraKabisa