Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imetoa ajira za kudumu kwa wahitimu 136 kutoka vyuo vikuu mbalimbali nchini kupitia programu ya mafunzo ya uzoefu wa kazi (Internship Program) katika kipindi cha miaka mitano iliyopita… hatua iliyofanya benki hiyo kushinda tuzo ya mwajiri bora katika programu hiyo iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano.
Tuzo hiyo imekabidhiwa jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano) Rahma Kisuo katika hafla iliyoshirikisha viongozi waandamizi wa serikali wakiwemo Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Zuhura Yunus, maofisa wa OWM-KAM pamoja na wawakilishi wa taasisi mbalimbali.
Kaimu Mkuu wa Idara ya Rasilimali Watu, Grace Mgondah amesema tuzo hiyo ni matokeo ya jitihada endelevu za benki hiyo katika kuwajengea wahitimu uzoefu na ujuzi wa kazi, jambo lililowasaidia wengi wao kupata ajira ndani na nje ya benki hiyo. Alisema kwa mwaka, wahitimu kati ya 800,000 hadi 1,200,000 huingia sokoni, lakini wengi hukosa uzoefu wa kazi, hivyo programu hiyo imekuwa daraja muhimu kati ya elimu na ajira.
#AzamTVUpdates
Mhariri | John Mbalamwezi