Dar es Salaam. Staa wa Bongofleva, Lava Lava kwa mara ya kwanza anauanza mwaka akiwa msanii huru anayejitegemea mara baada ya kuachana na WCB Wasafi, lebo iliyosimamia kazi zake kwa mafanikio makubwa tangu 2017.

Kwa sasa anajisimamia kimuziki kupitia lebo yake mpya, Bite Gang ambayo ina jukumu kubwa la kubadilisha na kuleta mweleko mpya wa mwanamuziki huyo katika soko la Bongofleva lenye ushindani.  

Hata hivyo, swali la wengi ni kwa namna gani Bite Gang itambadilisha mwimbaji huyo ikiwa WCB Wasafi yenye nguvu kubwa ya ushawishi ilishindwa kulikuza jina lake kwa ukubwa kama ilivyo kwa wenzake.

Lava Lava ni mwimbaji na mtunzi wa nyimbo anayesifika kwa sauti yake laini, yenye hisia na mvuto wa kipekee unaochanganya ladha ambayo inawavutia wasikilizaji wengi.
Kwa kutumia kipaji chake kikubwa amesimulia hadithi nyingi kupitia muziki akiimba nyimbo nzuri zinazogusa mada za mapenzi, starehe na maisha ya kila siku.

Alipata umaarufu mkubwa kupitia wimbo wake, Tuachane (2017), mradi wa kwanza chini ya WCB Wasafi na ndio uliomtambulisha na wengi wakakiri hiki ni kipaji kikubwa kitakachokuja kufanya makubwa.

Baada ya hapo alikuja kutamba na nyimbo nyingine kama Niuwe, Gundu, Basi Tu, Ng’ari Ng’ari, Habibi, Tuna Kikao, Saula, Kilio, Inatosha, Desh, Bado Sana, Go Gaga, Wanga, Tajiri, Kibango n.k.

Nyimbo hizi si tu zimempa umaarufu katika Bongofleva, bali mashabiki wengi kutoka ukanda mzima wa Afrika Mashariki huku zikithibitisha uwezo wake mkubwa wa kuwasiliana na mashabiki kupitia muziki.

EP yake ya kwanza, Promise (2021) yenye nyimbo nne huku ikiwashirikisha Mbosso na Diamond Platnumz, ilionyesha ukuaji wake wa kisanaa kama msimuliaji mahiri wa hadithi za mapenzi katika muziki wa Kiswahili.

Baada ya takribani miaka minane akiwa na WCB Wasafi, mnamo Juni 2015, Lava Lava akathibisha kuachana na lebo hiyo na kuanza safari mpya ya kimuziki akiwa na lebo yake, Bite Gang.

Mradi wa kwanza chini ya Bite Gang ni EP yake ya pili, Time (2025) yenye nyimbo sita huku akiwashirikisha Billnass na Yammi, mwimbaji wa zamani wa The African Princess, lebo yake Nandy.

Kupitia mchanganyiko wa melodi tamu, midundo yenye mvuto na mashairi yenye maudhui mazuri, kila wimbo katika EP hiyo inayozungumzia mapenzi na starehe, umebeba ujumbe wa kipekee kwa wasikilizaji.

Utolewaji wa EP hii unaashiria sura mpya katika safari ya muziki wa Lava Lava, na unaweka mwelekeo wa kile kinachotarajiwa chini ya Bite Gang, ikiwa kama lebo changa inayotaka kusimamisha himaya yake.

Hata hivyo, mapokezi ya EP hiyo hasa katika majukwaa ya kidijitali hayajawa makubwa kama ilivyotarajiwa, namba zake zipo chini sana, na hilo linaibua swali iwapo Bite Gang itaweza kumfikisha mbali staa huyo.

Mathalani hakuna wimbo hata mmoja ambao umesikilizwa hata walau mara milioni 1 katika mitandao yote iliyowekwa EP hiyo ikiwa ni zaidi ya miezi minne tangu kuachiwa kwake.

Ila hata kipindi yupo WCB Wasafi, nyimbo zake hazikuwa zikipata namba kubwa ukilinganisha na wasanii wengine wa lebo hiyo. Hivyo ilitarajiwa Bite Gang itaanza kulifanyia kazi hilo ila kwa jinsi ilivyoanza inatia shaka.

Hii ni tofauti na msanii mwenzake, Mbosso ambaye walioondoka wakati mmoja pale WCB Wasafi. Kwa upande wake Mbosso naye alianzisha lebo yake, Khan Music, kisha kutoa EP, Room Number 3 (2025).

EP ya Mbosso na nyimbo zake kama Pawa na Aviola, imefanya vizuri ikishika namba moja kwa mwaka 2025 katika mitandao ya Spotify na YouTube unaotumiwa na mashabiki wengi nchini.  

Kwa sasa kinachosubiriwa kutoka kwa Lava Lava ni singo ya kwanza nje ya EP yake, na hiyo inaweza kutoa picha halisi ni kwa kiasi gani amejipanga na Bite Gang yake.

Ikumbukwe mbali na Lava Lava na Mbosso, wanamuziki wengine waliowahi kusimamiwa na WCB Wasafi na sasa wana lebo zao, Rich Mavoko – Billionea Kid, Harmonize – Konde Music Worldwide na Rayvanny – Next Level Music (NLM).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *