Ikiwa ni katika fremu ya uingiliaji wake katika masuala ya ndani ya Iran, Rais Donald Trump wa Marekani amezindua sarakasi mpya ya takwimu kuhusu Iran.
Kwa mara nyingine tena, na ikiwa ni katika kuendeleza tabia yake ya kuingilia masuala ya ndani ya Iran, Rais wa Marekani amejaribu kubuni takwimu za kuhalalisha hatua yake hiyo, ikiwa ni pamoja na uwezekano wa kuchukua hatua za kijeshi, licha ya kukiri kwamba idadi ya watu waliouawa katika machafuko ya Iran haijulikani.
Trump pia amewataka washirika wa Marekani kuondoka Tehran kufuatia pendekezo la wizara ya mambo ya nje ya nchi hiyo ya kuwataka raia wa Marekani waondoke Iran. Matamshi yanayogongana na yasiyoeleweka vizuri ya Trump kuhusu machafuko ya Iran, kabla ya kahusiana na masuala ya kibinadamu na haki za binadamu, yanaashiria jaribio la serikali ya Marekani la kuzidisha na kukuza kupita kiasi idadi ya waliopoteza maisha katika ghasia za karibuni na hivyo kuweka msingi wa kuingilia na hata kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Iran. Wakati Trump anazungumza juu ya “kutokuwa na uhakika wa idadi ya waliokufa” wakati huo huo anazungumzia kusikia “idadi kubwa sana ya waliouawa”, mbinu inayochukuliwa kuwa sehemu ya mashinikizo ya kisiasa na propaganda za vyombo vya habari za Washington kwa ajili ya kuhalalisha hatua zake zilizo kinyume cha sheria dhidi ya Iran. Sisitizo lake la mara kwa mara juu ya takwimu ambazo hazijathibitishwa, pamoja na pendekezo la kuondoka raia wa Marekani nchini Iran, yote hayo yanaonyesha kuwa Ikulu ya White House inaandaa mazingira ya kijeshi dhidi ya Iran.
Siku ya Jumanne, Trump aliunga mkono waziwazi katika mtandao wa kijamii, kuendelea kwa machafuko na kuwachochea wananchi wa Iran wavamie taasisi za serikali, jambo ambalo ni mfano wa wazi wa uingiliaji wa moja kwa moja katika masuala ya ndani ya nchi huru.
Sambamba na sera ya mashinikizo ya juu dhidi ya Iran, rais huyo wa Marekani mwenye utata pia ameibua vitisho vipya dhidi ya nchi ambazo zina mabadilishano ya kiuchumi, kibiashara na nishati na Iran. Mnamo Januari 13, Trump alitangaza kuwa: “Kuanzia sasa, nchi yoyote ambayo inafanya biashara na Iran italipa ushuru wa asilimia 25 kwa aina yoyote ya biashara inayofanya na Marekani.”

Inaonekana kuwa hatua ya Rais wa Marekani kuangazia na kukuza kupita kiasi idadi ya watu waliouawa katika ghasia za Iran ina malengo kadhaa maalum. Moja ya malengo hayo ni kuongeza mashinikizo ya kimataifa dhidi ya Iran. Wakati Trump katika jumbe zake za mtandaoni anawachochea “Wairani waendelee kuandamana” na kuonya kwamba Tehran “italipa gharama kubwa”, jumbe hizi zinaweza kuchambuliwa katika muktadha wa kujaribu kuiondolea Jamhuri ya Kiislamu ya Iran uhalali wake kimataifa. Pia, kutia chumvi idadi ya vifo kunaweza kufanya maoni ya umma kimataifa kuzingatia zaidi hali ya Iran na hivyo kuandaa mazingira ya kuongezeka mashinikizo ya kisiasa au hata vitisho vya kijeshi dhidi yake.
Kwa upande mwingine, madai ya idadi kubwa ya watu waliouawa katika ghasia za Iran yanaweza pia kuwa na nafasi katika siasa za ndani za Marekani. Katika mazingira ambayo sera za nje ni mojawapo ya mihimili mikuu ya ushindani wa kisiasa, kudhihirisha uso wenye azma thabiti dhidi ya Iran kunaweza kuwa na umuhimu mkubwa wa kiuchaguzi kwa Trump. Katika muktadha huu, tovuti ya “Politico” imedai kwamba kufuatia vitisho vya Trump, Iran “iliomba kufanya mazungumzo”; madai ambayo yanaweza kutafsiriwa ndani ya Marekani kama ishara ya mafanikio ya mashinikizo yake.
Kwa ujumla tabia ya ghafla na isiyotabirika ya rais wa Marekani inaonyesha kuyumba kwa siasa za nje za utawala wake pamoja na jaribio la kushinikiza na kuibana Iran kufuatia vita vya siku 12. Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa mkanganyiko huo sio tu unadhoofisha sura ya Marekani katika uga wa kimataifa, bali pia unaonyesha kuwa sera za nje za Washington zimeundwa kwa msingi wa propaganda za vyombo vya habari na mashinikizo ya kisiasa, badala ya kuzingatia ukweli wa mambo na vilevile wasiwasi wa kibinadamu. Mtazamo huu unaonyesha kuwa, lengo kuu la Marekani si kuwaunga mkono wananchi wa Iran wakati wa machafuko ya hivi karibuni, bali ni kutumia vibaya hali hii kisiasa na kijeshi kupitia mashinikizo na kutekeleza siasa za upande mmoja dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.