Dar es Salaam. Zimebaki siku tisa kuanzia Februari 2, 2026 kwa Chama cha ACT Wazalendo, kuamua kuingia au kukacha kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), Zanzibar.

Siku tisa zilizobaki, ndizo zitakamilisha zile siku 90, ambazo kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 na marekebisho yake ya mwaka 2010, ACT Wazalendo ndicho kinachopaswa kuingia SUK.

Hata hivyo, Mwanasheria Mkuu wa ACT Wazalendo, Omary Issa Shaaban ameliambia Mwananchi Jumatano Januari 28,2026 kuwa hawana wasiwasi na siku 90 kwa sababu Katiba haijaweka shinikizo katika siku hizo.

Endapo siku hizo zikapita bila ACT Wazalendo kuingia SUK, itakuwa imefanya kama kile kilichofanywa na Chama cha Wananchi (CUF) Machi 2016 kiliposusia uchaguzi wa marudio.

Ingawa kuna tofauti, kwani ACT Wazalendo, kilishiriki uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025 na kuibuka nafasi ya pili baada ya mgombea wake, Othman Masoud kupata kura za urais 139,399 sawa asilimia 23.22 nyumba ya Dk Mwinyi aliyepata kura milioni 448,892.

Lakini mwaka 2016 kwenye uchaguzi wa marudio wa Zanzibar, viongozi wa CUF enzi hizo, kabla ya kuhamia ACT Wazalendo, wakiongozwa na Maalim Seif Sharif Hamad waligomea mchakato huo wakidai ni batili, ambapo Dk Ali Mohamed Shein aliibuka kidedea wa urais kwa kura 299,982, sawa na asilimia 91.4.

Aidha, katika kikao cha kamati kuu kilichoketi Januari 18, 2026 chama cha ACT Wazalendo kiliazimia kamati maalumu iliyoundwa kufanya tathimini ili kubaini kama malengo ya kuanzishwa SUK yanatimizwa au vinginevyo.

Akizungumza na Mwananchi Januari 28, 2026, kuhusu maendeleo ya kamati hiyo, Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo (Bara), Isihaka Mchinjita amesema inaendelea vizuri na majukumu yake na itafika mahali watatoa taarifa kwa umma.

“Kamati inaongozwa na watu watatu kwa hatua ya awali, jukumu lake ni kupigania haki zilizopokwa na zilizofanya SUK iwe na maana na kurejeshwa. Kwa sasa ni mambo ya ndani yanayoendelea, si kuyatoa nje.

“Hatujaweka wazi majina ya wajumbe, kwa sababu bado inafanya kazi ndani, lakini itafika mahali umma utajua, baada ya hatua fulani kufikiwa,” ameeleza Mchinjita.

Ufafanuzi wa kikatiba  

Katika ufafanuzi wake, Omary anaeleza Katiba ya Zanzibar imeeleza dhana ya siku 90 kuhusu SUK, katika Ibara ya 42 (A).

Kwa mujibu wa Omary, ibara hiyo inampa Rais wa Zanzibar siku 90 kujaza nafasi za SUK, iwapo Makamu wa Kwanza wa Rais au mawaziri wanaotokana na upinzani wamejiuzulu au kuacha kutekeleza kazi zao kwa zaidi ya siku saba.

Katika ufafanuzi wake, amesema Katiba haimpi Rais wa Zanzibar siku 90 kuwa ukomo kwa chama kilichokuwa nafasi ya pili katika uchaguzi kupeleka jina la Makamu wa Kwanza wa Rais.

“Na iwapo nafasi hizo zitakuwa wazi zaidi ya siku 90, Rais anaweza kuteua mawaziri wengine kujaza nafasi hizo. Dhumuni la siku 90 ni pale ambapo unaye makamu wa kwanza na mawaziri ambao wamejiuzulu au kuacha kazi zao,” amesema.

Omary anafafanua ibara ya 39 (A)1, inasema endapo ndani ya siku saba, baada ya Rais kushika madaraka chama kinachostahiki kutoa makamu wa kwanza na kitashindwa kuwasilisha kwa Rais jina la uteuzi, Rais bila kujali masharti ya 39 (1 na 3) ya Katiba ataacha wazi nafasi hiyo na kuteua makamu wa pili.

“Halafu kifungu cha 39 (A) 2 kinasema kwa mujibu wa masharti ya kifungu cha kwanza cha kifungu hiki, Rais bila kujali kifungu cha 42(2) cha Katiba atateua mawaziri na kuacha wazi nafasi ya uteuzi ya chama au vyama vya upinzani, imeishia hapo haijatoa muda wa nafasi kujazwa.

“Hii hoja ya siku 90 inatokea wapi? Hatufanyi kazi kwa presha ya siku 90. Hatuna presha ya kikatiba na Rais hana hiyo presha ya kikatiba ya kujaza ndani ya siku 90,” ameeleza Omary.

Alichokisema mwanasheria

Kama ilivyoelezwa na Omar, mmoja wa wanasheria waandamizi wa Zanzibar, Hassan Kijogoo, anasisitiza hilo, akisema Katiba inamtaka Rais kuacha wazi nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais na mawaziri iwapo chama kinachostahili kupata nafasi hizo hakikupeleka jina.

“Sasa suala la kujiuliza baada ya siku saba nafasi imeachwa wazi, wanaweza kupeleka jina? Katiba imekaa kimya na kama imekaa kimya tafsiri yake ni kwamba sio dhambi kupeleka hilo jina baada ya siku saba kuisha hata mwaka endapo watajisikia,” amesema.

Jitihada zilizofanyika ACT kuingia SUK

Baada ya kuapishwa na kuanza kutekeleza majukumu yake ya muhula wa pili, Dk Mwinyi alisikika akisema yupo tayari kutekeleza maridhiano kwa mustakabali wa wananchi wa Zanzibar.

Katika kufanikisha hilo, tayari Rais Mwinyi ameacha nafasi nne za mawaziri zinazotakiwa kujazwa na wawakilishi wanaotoka ACT Wazalendo, kwa mujibu wa mgawanyo wa idadi ya viti vilivyopatikana.

Wizara hizo ni pamoja na Wizara ya Afya, Maliasilia na Mambo ya Kale, Biashara na Maendeleo ya Viwanda na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.

Kama hiyo haitoshi, kumekuwa na juhudi mbalimbali za mazungumzo ya maridhiano yanayoendelea yanayoongozwa na viongozi wastaafu wa Zanzibar, wakikutana kwa nyakati tofauti na ACT Wazalendo ili kusaka mwafaka.

Kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, inataka chama au vyama vya upinzani ambavyo vimepata wajumbe kwenye Baraza la Wawakilishi tuwapatie nafasi katika Baraza la Mawaziri.

“Chama pekee kilichopata viti ni ACT Wazalendo, wamepata viti 10, ukizidisha hiyo kwa idadi ya wizara 20 unapata 200, ukigawa kwa majimbo 50, unapata nne. Kwa hiyo nafasi zao kwenye baraza la mawaziri nne,” alisema Rais Mwinyi.

“Nimeamua kuziacha wazi nafasi za uteuzi nne hadi tutakapokubaliana aidha wanaingia SUK au la. Hapa natumia mamlaka yangu ya kikatiba hizi nafasi zitabaki wazi kwa mujibu wa katiba hadi pale kipindi kitakapoisha ambacho ni siku 90,” alieleza Dk Mwinyi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *