
CHAMA Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga kimepiga marufuku tabia ya baadhi ya viongozi kulalamika badala ya kutatua changamoto za wananchi, kikiwataka kuchukua hatua za haraka na madhubuti kumaliza kero zinazowakabili wananchi.
Agizo hilo limetolewa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Rajab Abdurahman, wakati wa ziara ya kukagua utekelezaji wa maagizo ya usafi katika soko la Mgandini. Amesema kazi ya msingi ya kiongozi ni kutafuta suluhu ya changamoto za wananchi na si kuwa sehemu ya malalamiko. “Tanga tunahitaji viongozi wenye uwezo wa kuondoa changamoto za wananchi. Kazi ya kiongozi ni kuchukua hatua ili kumaliza kero si kulalamika,” amesema. SOMA: ‘Muwe mabalozi wa amani’
Hata hivyo, amewataka viongozi hao kuja na mipango madhubuti ya muda mrefu itakayohakikisha usafi wa mazingira unaimarika pamoja na kuboreshwa kwa miundombinu ya majitaka katika maeneo ya biashara. Akijibu maelekezo hayo, Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga, Seleboss Mustafa, amesema tayari wameanza kutekeleza mikakati hiyo kwa vitendo ili kuboresha hali ya usafi katika jiji hilo.