Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imefanya mabadiliko makubwa ya safu ya uongozi wake wakiwamo makamisha na wakurugenzi wa idara.

Viongozi hao wapya wameteuliwa hivi karibuni na Bodi ya Wakurugenzi chini ya Mwenyekiti wake, Uledi Mussa Abasi ambako wanatarajiwa wanataimarisha utoaji wa huduma bora kwa walipakodi sambamba na kupanua wigo wa kodi nchini.

Akizungumza wakati wa kuwatambulisha viongozi hao kwa watumishi wa TRA,jijini Dar es Salaam, Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Juma Mwenda amesema uteuzi huo unalenga kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato pamoja na kuhakikisha haki na usawa katika mfumo wa kodi.

Viongozi waliotambulishwa ni pamoja na Michael Muhoja, aliyekuwa akihudumu katika Idara ya Walipakodi Wakubwa na sasa amehamishiwa kuwa Kamishna wa Idara ya Kodi za Ndani, pamoja na Edmund Kawamala aliyeteuliwa kuwa Kaimu Kamishna wa Idara ya Walipakodi Wakubwa.

Kamisha Mwenda amewataka viongozi hao kusimamia kwa umakini suala la usawa katika utozaji wa kodi, akisisitiza umuhimu wa kutoa motisha kwa walipakodi ili kuchochea ulipaji wa kodi kwa hiari. Amesema kwa sasa idadi ya walipakodi nchini ni milioni nane pekee ambayo ni ndogo ikilinganishwa na idadi ya Watanzania wenye uwezo wa kufanya kazi.

Wengine walioteuliwa ni Eva Raphael Magoti, aliyekuwa Meneja wa TRA Mkoa wa Kodi Ilala, ambaye sasa ni Kaimu Naibu Kamishna Uendeshaji wa Idara ya Walipakodi Wakubwa, pamoja na Specioza Mickness Owure, aliyekuwa Meneja wa TRA Mkoa wa Njombe, aliyeteuliwa kuwa Kaimu Naibu Mkurugenzi wa Mipango.

Kwa upande wao, viongozi hao wapya wameahidi kuimarisha ushirikiano na walipakodi, kuongeza elimu ya kodi kwa umma, kupanua wigo wa kodi na kuhakikisha huduma bora pamoja na usawa katika ulipaji wa kodi nchini.

(Feed generated with FetchRSS)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *