DAR ES SALAAM: Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima, amekemea vikali uzushi unaosambaa kuwa mwanaume akishikwa begani hupoteza sehemu zake za siri, akieleza kuwa taarifa hizo ni za uongo mtupu na upotoshaji.
Ametoa kauli hiyo katika Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto Anayeishi na Kufanya Kazi Mtaani yaliyofanyika Wilaya ya Ubungo, Dar es Salaam, yakilenga kuhamasisha ulinzi, malezi na ustawi wa watoto.

Katika tukio hilo, Waziri Gwajima ameamsha ari kwa wanaume kushiriki kwa vitendo kushikana mabega kuonesha ukweli, ambapo walifanya zoezi la kushikana mabega wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando. Baada ya zoezi hilo, ilithibitishwa wazi kuwa taarifa hizo ni uzushi, kwani hakuna aliyepoteza sehemu zake za siri.
Aidha, amewataka wananchi kupuuza taarifa za aina hiyo na kujikita katika shughuli za maendeleo, huku akisisitiza umuhimu wa jamii kuwa na uelewa sahihi wa kupambanua taarifa za kweli na za upotoshaji.

Katika hatua nyingine, ameelekeza viongozi wa wizara kuongeza kasi ya utoaji elimu kwa umma ili kuondoa dhana potofu zinazoweza kupotosha jamii na kudhoofisha ajenda za maendeleo.