
Uchokozi wa Marekani na Israel dhidi ya Iran katika Vita vya Ramadhani na ukosefu wa usalama katika Mlango-Bahari wa Hormuz na kuzingirwa kwake na Marekani, ambayo ndiyo njia kuu ya kupitisha nishati na vifaa vya matibabu kote duniani, kumezidisha mgogoro wa binadamu nchini Sudan.
Televisheni ya Al Jazeera ya Qatar imeripoti kuwa, hali ya nyanjani nchini Sudan inaonyesha mgogoro maradufu wa binadamu kufuatia kuyumba usalama wa Mlango-Bahari wa Hormuz, na kwamba raia wa nchi hiyo, wanaosumbuliwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe, wanakabiliwa na hali mbaya ya kiafya inayotokana na mvutano wa kijeopolitiki uliosababishwa na Marekani na Israel katika Mashariki ya Kati.
Ripoti hiyo imeongeza kuwa, athari mbaya za Vita vya Ramadhani dhidi ya Iran katika eneo la Mashariki ya Kati haziishii katika kukata njia za usafirishaji wa meli na kusababisha mgogoro wa nishati duniani, lakini pia zimepunguza sana uwezo wa mashirika ya misaada kupeleka chakula na dawa kwa mamilioni ya watu wanaohitaji kote duniani, huku Sudan ikiwa juu katika orodha ya nchi zilizoathiriwa zaidi.
Katika muktadhaa huo, mateso ya kila siku ya watu wa Sudan yanahusishwa na uhaba mkubwa wa dawa. Raia mmoja wa Sudan anaelezea ukweli huu mchungu akisema: “Wakati mwingine tunakuwa na dozi chache tu za kifurushi cha dawa, na tunajaribu tuwezavyo kupata dawa zaidi, lakini mara nyingi tunashindwa kupata dawa.”
Umoja wa Mataifa umeonya kuhusu kuzorota zaidi hali mambo nchini Sudan, ukiashiria ongezeko la 20% la gharama za usafirishaji duniani na ucheleweshaji wa kuwasili bidhaa mbalimbali unaosababishwa na njia mpya za usafirishaji wa bidhaa.