Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mwabwola, iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, wamelalamikia ukosefu wa huduma ya maji safi na salama, hali inayowaathiri katika utekelezaji wa shughuli zao za kila siku.

Kutokana na changamoto hiyo, hulazimika kutumia maji ya madimbwi pamoja na ya mvua yanayohifadhiwa kwenye matanki kwa matumizi mbalimbali, ikiwemo usafi wa vyoo, madarasa na ofisi, pamoja na umwagiliaji wa miti kama sehemu ya juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Imeelezwa kuwa shule hiyo hutegemea majaba na matanki kuhifadhi maji wakati wa msimu wa mvua, lakini kiwango hicho hakitoshelezi mahitaji ya kila siku.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Jumapili, Aprili 26, 2026, Makamu Mkuu wa shule hiyo, Abel Medard, amesema shule haina miundombinu ya uhakika ya maji safi na salama, jambo linalowalazimu wanafunzi kubeba maji kutoka nyumbani ili kuyahifadhi shuleni kwa matumizi ya kawaida.

Wanafunzi wa Chuo cha mtakatifu Augustino Mwanza (SAUT)wawili kutoka kulia na mwanafunzi wa Shule ya Mwabwola Sekondari kutoka kulia wakipanda mti katika shule hiyo iliyo Wilaya ya Kwimba, Mkoa wa Mwanza.

“Wanafunzi hulazimika kuleta maji kutoka nyumbani na kuyahifadhi kwenye matanki ya shule. Wakati mwingine hulazimika pia kutumia maji ya madimbwi yaliyopo jirani kwa ajili ya shughuli kama umwagiliaji wa miti,” amesema Medard.

Ametoa wito kwa Serikali kuchukua hatua za haraka kuhakikisha shule hiyo inapata huduma ya maji safi na salama, ili kurahisisha utoaji wa huduma na kuzuia magonjwa ya mlipuko yanayoweza kusababishwa na matumizi ya maji yasiyo salama.

Kwa upande wao, wanafunzi wameeleza kuwa hali hiyo inaathiri hata utekelezaji wa miradi ya mazingira, hususan upandaji na utunzaji wa miti.

Cleopatrah Rashid, mwanafunzi wa kidato cha pili, amesema wanalazimika kubeba maji kutoka nyumbani au kutumia maji ya madimbwi ili kumwagilia miti, jambo linalopunguza ufanisi wa juhudi hizo.

Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari Mwabwola, Abel Medard akiwa akipanda mti katika shule ya Mwambola Sekondari iliyopo halmashauri ya Wilaya ya Kwimba, Mkoa wa Mwanza.

Naye Thomas Hassan, mwanafunzi wa kidato hicho, amesema upandaji miti shuleni hapo unalenga kusaidia upatikanaji wa mvua na kuboresha mazingira, lakini changamoto ya maji inakwamisha jitihada hizo.

Katika hatua ya kuhamasisha utunzaji wa mazingira, wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT) Mwanza, kwa kushirikiana na shule hiyo na Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, wameshiriki upandaji miti 800 katika eneo hilo.

Akizungumza wakati wa upandaji miti, Mhadhiri Mwandamizi kutoka Shule ya Mawasiliano na Uandishi wa Habari ya SAUT, Aneth Nkeni, amesema lengo la ushiriki wao ni kuwajengea wanafunzi uwezo wa kuwajibika kwa jamii na kushiriki katika shughuli za maendeleo.

Mwanafunzi wa SAUT, Sosoma Emmanuel, amesema upandaji miti ni njia ya kuenzi Taifa kwa kutunza mazingira na kusaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, huku Sabitina Haruni akisisitiza kuwa miti hiyo itasaidia kurejesha uoto wa asili katika eneo linalokabiliwa na ukame.

Shule ya Mwabwola Sekondari iliyopo Wilaya ya Misugwi, Mkoani Mwanza.

Mbali na upandaji miti, tukio hilo pia limejumuisha shughuli nyingine za kijamii, zikiwemo uchangiaji damu, mbio za pamoja na bonanza la michezo mbalimbali kama mpira wa miguu, mpira wa pete na mpira wa wavu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *