
Dodoma. Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imetaja mojawapo ya changamoto zilizokwamisha bajeti ya 2025/26 isiweze kutekelezwa ni kuwepo kwa baadhi ya nchi katika Jumuiya kutoheshimu mikataba ya makubaliano ikiwemo la kulipa michango.
Kauli hiyo imetolewa leo Ijumaa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya ushirikiano wa Afrika Mashariki James Millya wakati akifungua mkutano wa Baraza la wafanyakazi wa Wizara hiyo.
Millya amesema hatua hiyo iliathiri uratibu na ushiriki wa Tanzania katika utekelezaji wa programu za mtengamano wa kikanda kwa baadhi ya wadau ikiwemo sekta binafsi.
Naibu Waziri ametaja sababu za kuzorota kwa hali ya amani na usalama kwa baadhi ya nchi ndani na nje ya ukanda wa Afrika na hivyo kuathiri utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001, Toleo la Mwaka 2024.
“Hali hii imepelekea kutotabirika kwa mwelekeo wa sera katika uhusiano wa kimataifa na kasi ndogo ya nchi wanachama kuridhia na kutekeleza Makubaliano ya Kikanda na hivyo kusababisha kuchelewa kufanikisha malengo ya Mtangamano wa Kikanda,” amesema Millya.
Mbunge huyo wa zamani wa Afrika Mashariki amesema ili kukabiliana na hali hiyo, Wizara imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kushirikiana na wadau wengine ndani na nje ya Serikali na inapolazimu kuhimiza matumizi ya vikwazo vilivyowekwa.
Kingine amesema Wizara imeendelea kuratibu na kushiriki kikamilifu katika kuunga mkono juhudi za Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa kuleta suluhu ya migogoro kwa njia za kidiplomasia.
Waziri ameagiza baraza kuwashirikisha watumishi katika mipango kwani inasaidia kupata mawazo mapya, lakini unawahusisha watumishi moja kwa moja kuhakikisha mipango iliyowekwa inatekelezwa.
“Kikubwa twendeni tukawahimize watumishi wenzetu kujituma na kuondoana na uzembe na vitendo vya rushwa mahali pa kazi, lakini nitilie mkazo katika uwajibikaji kwa watumishi ili kuongeza tija na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara,” amesema.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo, kufanya kazi kwa kusukumana na kusimamiana siyo jambo jema kwani kila mmoja anapaswa kuona fahari kufanya kazi katika wizara hiyo nyeti ili mwisho wa utumishi wake aache alama.