
Dodoma. Sheria ya ndoa ya mwaka 1971 bado inawapasua vichwa wabunge, lakini Serikali imepanga kuendelea kupokea maoni kutoa kwa wananchi mikoani.
Mara kadha hoja hiyo imekuwa ikiinuka kwa baadhi ya wabunge kutaka ifanyiwe marekebisho hasa kifungu cha 13.
Mbunge wa Viti Maalumu, Taska Mbogo ameuliza lini Serikali itarekebisha kipengele cha 13 cha Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 ambacho kinaruhusu mtoto wa kike kuolewa na umri wa miaka 15.
Katika swali la nyongeza, Mbogo amehoji ni kwa nini Serikali inaweka ubaguzi katika sheria za nchi na kukinzana na Katiba ya nchi ambayo inataja umri wa mtu mzima ni miaka 18 wakati mtoto wa kike bado anaruhusiwa kuolewa akiwa na miaka 15.
Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Zainabu Katimba amesema Sheria ya Ndoa, Sura 29 wakati inatungwa mwaka 1971 ilitanguliwa na ukusanyaji wa maoni kwa jamii kwa njia ya ‘White paper’ ambapo Watanzania wote walishirikishwa kutokana na Sheria hii kuwa na uhusiano wa moja kwa moja wa imani za dini na tamaduni.
Naibu Waziri amesema tangu Sheria hii itungwe, imeshafanyiwa marekebisho mara nne mwaka 1972, 1980, 1996 na 2006.
“Mheshimiwa Spika, Serikali ilikusanya maoni katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Mtwara, Lindi, Arusha, Dodoma na Mara kuhusu Sheria ya Ndoa, Sura 29,” amesema Katimba.
Hata hivyo, ameliambia Bunge kuwa, baada ya uchambuzi wa maoni yaliyokusanywa imeonekana kuna hitaji la kukusanya maoni zaidi katika mikoa iliyosalia, zoezi ambalo limepangwa kuanza katika mwaka wa fedha wa 2026/2027. Mara baada ya kukamilika kwa zoezi hilo.
Amesema Serikali itawasilisha bungeni muswada huo ukiwa umezingatia maoni ya wananchi.