Dar es Salaam. Kama ni mfuatiliaji wa mitandao ya kijamii, bila shaka utakuwa umekutana na habari kuhusu muigizaji wa tamthilia, Vanessa Kashera maarufu kama ‘Vee’, ambaye pia ni mzazi mwenza wa nyota wa zamani wa Yanga, Stephane Aziz KI kudaiwa kuwa ni mjamzito wa mchezaji wa Simba SC, Morice Abraham.
Madai hayo yamesambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii huku baadhi ya watu wakisema huenda ndio chanzo cha Aziz KI kuachana kwa Vanessa, kabla ya mwanasoka huyo kuhamishia kambi kwa Hamisa Mobetto ambapo sasa ni mke na mume.
Akizungumza na Mwananchi, Vanessa amesema ni kweli ana ujauzito na anatarajia kupata mtoto, lakini si wa Morice Abraham kama watu wengi wanavyodai.
Vanessa ameeleza kuwa, Morice ni mtu wa karibu katika familia yao na hata humuita shemeji yake, huku akisisitiza kuwa taarifa zinazoenezwa mitandaoni si za kweli.
“Ni kweli nina ujauzito, lakini si wa Morice Abraham kama watu wanavyosema. Morice ni shemeji yangu na ni mtu wa karibu sana kwangu,” amesema Vanessa.
Vanessa anatarajia kupata mtoto wake wa pili baada ya wa kwanza kuzaa na Aziz KI kipindi wapo katika mahusiano, huku mjadala kuhusu ujauzito wake wa sasa ukiendelea kuzua gumzo kubwa kwenye mitandao ya kijamii wengi wakitaka kumfahamu baba mtoto ambapo mwenyewe hakuwa tayari kumuweka hadharani.
