Lango Bahari la Hormuz takriban limefungwa kwa wiki nne sasa na hivyo
kupelekea soko la mafuta duniani kutumbukia katika mgogoro mkubwa wa nishati na wala haijulikani litafunguliwa lini.
Vitisho na mashambulizi ya Iran dhidi ya meli za maadui zinazokataa kutii sheria katika Ghuba ya Uajemi yameongeza hatari ya kupita meli katika lango bahari hili na hivyo kupunguza pakubwa idadi ya meli za mafuta zinazopita katika njia hiyo nyembamba ya majini, ambayo ni mfereji mkuu unaotumika kusafirisha takriban asilimia 20 ya mafuta na gesi asilia duniani, pamoja na mbolea zinazosaidia kukuza mazao mbalimbali muhimu ulimwenguni.
Huku mzozo wa nishati ukizidi kuongezeka, Rais Donald Trump wa Marekani amedai kuna juhudi za kidiplomasia zinazoendelea kwa ajili ya kumaliza mzozo huo, huku pia akiendelea kutekeleza mipango ya kutuma maelfu ya wanajeshi wa Marekani katika Mashariki ya Kati kwa madai ya kufungua lango hilo na kusindikiza meli za mafuta katika eneo.
Lakini Iran bado ina nafasi nzuri ya kudhibiti Lango Bahari la Hormuz, kwa njia nyingi tu. Moja ya njia hizo ni matumizi yake ya mbinu za kivita visivyo na uwiano, ikiwa ni pamoja na matumizi ya droni za bei nafuu na mabomu ya baharini. Fursa muhimu zaidi kwa Iran ni nafasi yake ya kijiografia katika eneo. Kwa pamoja, mambo haya yanafanya iwe vigumu kwa Marekani au nchi nyingine yoyote yenye nguvu duniani kuweza kulinda meli za mizigo au kudhibiti kijeshi njia hiyo ya baharini.
Bila shaka kuna faida kubwa kwa Iran kuendelea kudumisha udhibiti wake katika eneo hili nyeti la uchukuzi majini. Viongozi wa Iran wamesema wataendelea kutoza ada kwa ajili ya kupita salama meli za mafuta kwenye Lango Bahari la Hormuz, baada ya ripoti ya shirika la Lloyd kusema Machi 23 kwamba, meli mbili zililazimika kulipa ada kubwa kabla ya kuruhusiwa na Iran kupita katika lango hilo.
Lango Bahari la Hormuz lina upana wa karibu maili 24 katika sehemu yake nyembamba zaidi, na wala hakuna njia nyingine mbadala kwa ajili ya meli kupita katika maji hayo. Hivyo Iran haipati usumbufu wa kuwinda na kufuatilia meli za mafuta bali kazi yake ni kuketi na kusubiri meli hizo zifike eneo la udhibiti wake.
Bila kusahau, Iran ina ukanda wa pwani wenye urefu wa karibu maili 1,000, ambao unaweza kutumika kwa ajili ya kuvurumisha makombora ya kulipua meli. Mitambo ya kuvurumisha makombora hayo inahamishika, na hivyo kuifanya kuwa ngumu kushambuliwa na adui. Ukanda huu mrefu wa pwani katika Ghuba ya Uajemi unamaanisha kuwa Iran inaweza kushambulia kirahisi hata meli za adui zilizo mbali zaidi ya Lango Bahari la Hormuz.

“Katika upande wa kaskazini wa Iran, sio eneo tambarare. Kuna miinuko, milima, mabonde, maeneo yaliyojengwa na visiwa vya pwani. Hayo yanafanya kugundulika tishio linalokaribia kuwa suala gumu zaidi na kuirahisishia Iran fursa ya kuficha mifumo yake inayohamishika ya silaha.
Wataalamu wa Magharibi watahadharisha kwamba hatari kubwa zaidi kutoka upande wa Iran ni matumizi yake ya silaha hatari zenye gharama ndogo ikiwa ni pamoja na droni, boti zinazokwenda kwa kasi kubwa na hata boti zisizo na nahodha zilizojazwa vilipuzi. Wanasema Iran pia ina nyambizi nyingi ndogo zinazoweza kutumika dhidi ya adui kwenye maji ya kina kifupi.
Katika siku za karibuni Iran imeshambulia takriban meli 20 karibu na Lango-Bahari la Hormuz, katika Ghuba ya Uajemi na katika Bahari ya Oman.
Wachambuzi wanaamini kuwa Iran hata haihitaji kushambulia meli ili kufanikiwa katika lengo lake la kuvuruga biashara ya nishati duniani. Maadamu tishio linabakia kuwa juu vya kutosha, makampuni ya usafirishaji na uchukuzi hayawezi kuhatarisha shughuli zao na kutia mkono gizani kwa kuanzisha tena safari za meli za mizigo katika eneo hili hatari kwa sasa. Baadhi ya meli za nchi zilizo na uhusiano mzuri na Iran, kama vile Uchina, India na Pakistan zimeruhusiwa kupita salama katika Lango Bahari la Hormuz.
Iran imesema “meli zisizo na uhasama” zinaweza kupita kwenye lango hilo kwa sharti zishirikiane na mamlaka ya Iran. Ripoti ya Lloyd’s List Intelligence imesema meli zisizopungua 16 zimefanikiwa kupita kwenye lango hilo, ikiwa ni pamoja na ile inayoaminika kulipa ada ya $ 2 milioni.
Hata kama meli zote za mafuta zitaanza tena kupita, ni wazi kuwa itachukua muda mrefu kabla ya kuondolewa mrundikano wa meli zinazosubiri nyuma ya lango hilo, kwa kutilia maanani kwamba meli zisizopungua 2,000 zimenasa ndani ya Ghuba ya Uajemi, kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Baharini.
Utawala wa Trump umekuwa ukipigia debe kile unachosema ni maendeleo katika juhudi za kidiplomasia, huku Iran, ikisisitiza kuwa haishiriki katika mazungumzo yoyote na Marekani, ingawa imekubali kubadilishana jumbe kupitia wapatanishi.