
KAIMU Kocha Mkuu wa Tausi FC, Martin Hammel amesema licha ya timu hiyo kuonyesha kiwango kizuri uwanjani, bado kuna maeneo kadhaa yanahitaji maboresho kabla ya kurejea kwenye mechi zijazo.
Akizungumza kuhusu mwenendo wa timu hiyo, Hammel amesema Tausi FC imekuwa ikifanya vizuri katika eneo la kushambulia na kukaba, hali inayowapa matokeo chanya, lakini bado wanahitaji kuongeza umakini.
“Tunacheza vizuri zaidi kwenye kushambulia na kukaba na matokeo tunapata, lakini tunahitaji kuboresha vitu vingi kabla hatujarudi tena uwanjani kwenye mechi zijazo,” amesema Hammel.
Kocha huyo amefafanua ligi imekuwa na ushindani mkubwa, hivyo ni muhimu kwa timu hiyo kuendelea kujipanga ili kuongeza zaidi kiwango cha timu.
Mbali na hilo, Hammel amezungumzia ushirikiano wa kimataifa kati ya Tausi FC na Tenerife Femenino inayoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake Hispania na hatua hiyo ni muhimu katika safari ya maendeleo ya klabu hiyo.
“Tunafurahia sana ushirikiano huu muhimu kati ya Tausi FC na Tenerife Femenino, kwani ni hatua kubwa katika ukuaji na maendeleo ya timu yetu. Utaleta fursa za kujifunza, maendeleo ya wachezaji na kubadilishana maarifa kati ya klabu zote mbili,” ameongeza.
Tausi FC iko nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi, imecheza mechi 14 ikishinda sita, sare tatu na kupoteza tano ikikusanya pointi 18.