Chama cha Wanasheria wa Afrika (Palu) kimewasilisha shauri jipya katika Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR), kikitaka ufafanuzi wa kisheria kuhusu wajibu wa nchi za Afrika katika kuhakikisha uwajibikaji kwa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.

Kinadai kuwa kwa miongo kadhaa, bara hilo limekumbwa na matukio hayo huku kukiwa na ukosefu wa uwajibikaji, na mara nyingi waathiriwa wameachwa bila haki huku wahusika wakiepuka mkono wa sheria.

Hatua hiyo inalenga kujibu swali la muda mrefu barani Afrika kuhusu namna bora ya kuhakikisha wahusika wa uhalifu mkubwa, ikiwemo ukiukwaji wa haki za binadamu na za jamii, wanawajibishwa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Jumamosi, Aprili 25, 2026, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Palu, Donald Deya, amesema chama hicho kimewasilisha rasmi ombi la maoni ya ushauri ili kupata mwongozo wa wazi wa kisheria kuhusu hatua zinazopaswa kuchukuliwa na nchi wanachama dhidi ya uhalifu mkubwa.

Ametaja baadhi ya makosa yanayolengwa kufafanuliwa kuwa ni mauaji ya kimbari, uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya ubinadamu na vitendo vingine vikubwa vya kikatili vinavyofanywa dhidi ya makundi ya watu.

Deya amesema historia ya Afrika imekumbwa na matukio mengi ya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, hasa wakati wa migogoro, hali iliyosababisha madhara makubwa kwa jamii na taasisi zake.

Hata hivyo, amebainisha kuwa kuna changamoto ya muda mrefu ya ukosefu wa uwajibikaji, na waathirika wengi wameachwa bila haki huku wahusika wakikwepa mkono wa sheria.

“Kwa miongo kadhaa, Bara la Afrika limepitia matukio ya kusikitisha ya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, yakiwemo mauaji ya kimbari na migogoro mingine, ambayo yameacha athari kubwa kwa jamii,” amesema Deya.

Ameongeza kuwa mara nyingi mifumo ya kisheria, iwe ya kitaifa, kikanda au kimataifa, imeshindwa kuhakikisha uwajibikaji kwa wakati na kwa ufanisi, jambo linalochangia kuendelea kwa tatizo hilo.

Katika muktadha huo, amesema kanuni ya mamlaka ya ulimwengu imekuwa chombo muhimu katika kupambana na kutowajibika, kwa kuwa baadhi ya uhalifu huchukuliwa kuwa wa kugusa ubinadamu wote na hivyo haupaswi kuzuiliwa na mipaka ya nchi.

Deya ametoa mfano wa kesi ya aliyekuwa Rais wa Chad, Hissène Habré, aliyekimbilia Senegal baada ya kuondoka madarakani.

“Waathiriwa wa utawala wake, kwa kushirikiana na asasi za kiraia, walichochea juhudi za kumfikisha mahakamani kwa tuhuma za mateso na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu,” amesema.

Amesema licha ya Senegal kusita mwanzoni, Ubelgiji ilianzisha uchunguzi kwa kutumia kanuni ya mamlaka ya ulimwengu na kuomba Habré arejeshwe ili ashtakiwe.

“Hali hiyo ilisababisha mgogoro wa kisheria uliowasilishwa katika Mahakama ya Haki ya Kimataifa (ICJ), ambayo iliamua kuwa Senegal ilikuwa na wajibu wa kumshitaki au kumkabidhi kwa mamlaka nyingine kwa mujibu wa mkataba dhidi ya mateso, na hatimaye Habré alishtakiwa na kuhukumiwa kupitia chombo maalumu cha Kiafrika,” amesema Deya.

Amebainisha kuwa tukio hilo si la kipekee, akitolea mfano pia juhudi za kimataifa baada ya mauaji ya kimbari nchini Rwanda.

Amesema baadhi ya wahusika walishtakiwa kupitia Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ya Rwanda (ICTR).

Hata hivyo, amesema mifano mingi ya uwajibikaji imechochewa na mataifa ya nje ya Afrika, badala ya kuwepo mfumo madhubuti wa pamoja wa Kiafrika.

Kutokana na hali hiyo, amesema PALU inalenga kupata ufafanuzi wa majukumu ya nchi wanachama chini ya Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu.

Amefafanua kuwa maswali yaliyowasilishwa mahakamani yanahusu iwapo nchi zina wajibu wa moja kwa moja kushtaki watuhumiwa wa uhalifu mkubwa, namna ya kushirikiana katika kuhakikisha haki inatendeka na iwapo majukumu hayo yanaweza kuvuka mipaka ya kitaifa.

Kwa mujibu wa Palu, ombi hilo halilengi kuanzisha sheria mpya, bali kufafanua wajibu uliopo ili utekelezwe kwa ufanisi katika bara zima.

Hatua hiyo inatarajiwa kuimarisha mifumo ya uwajibikaji na kuhakikisha wahusika wa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu wanachukuliwa hatua stahiki, huku waathiriwa wakipata haki zao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *