
Dar es Salaam. Wakati Rais wa Marekani, Donald Trump na ujumbe wake wakiwasili Beijing leo Mei 13,2026 kwa ajili ya mkutano wa ngazi ya juu na Rais wa China, Xi Jinping imeelezwa kuwa miongoni mwa ajenda nzito zitakazojadiliwa ni za kisiasa, kiuchumi na kiusalama.
Ziara hiyo ya siku mbili iliyoanza leo na kukamilika kesho Mei 14, 2026 Trump anakutana na Rais Jinping kupunguza mvutano wa biashara kati ya mataifa hayo mawili, makubaliano ya ushuru na vikwazo vya kiuchumi pamoja na ushirikiano wa kimkakati duniani.
Kwa mujibu wa The Guardian mazungumzo yatajikita zaidi katika juhudi za kuimarisha tena uhusiano wa mataifa hayo mawili makubwa kiuchumi duniani.
Mkutano huo wa siku mbili unakuja katika kipindi ambacho dunia inakabiliwa na changamoto za kisiasa na kiusalama, ikiwemo vita vinavyoendelea katika eneo la Iran na Ukraine, hali inayoongeza presha katika mazungumzo ya viongozi hao.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ikulu ya White House, Trump ameambatana na ujumbe wa wafanyabiashara wakubwa zaidi ya 12, wakiwemo Elon Musk wa Tesla na Tim Cook wa Apple, hatua inayoashiria umuhimu wa ajenda ya uchumi kati ya nchi hizo mbili licha ya mvutano wa kimkakati.
Vyanzo vya kidiplomasia vinaeleza kuwa mgogoro wa Mashariki ya Kati, hususan vita vinavyoendelea kati ya Marekani na Iran, unatarajiwa kuwa na athari kubwa katika mazungumzo hayo.
Licha ya mazungumzo ya awali ya kupunguza ushuru wa biashara, Marekani na China bado zipo katika hali ya tahadhari ya kiuchumi baada ya miaka ya mvutano wa kibiashara.
Washington inaituhumu Beijing kwa kuwa na ziada kubwa ya kibiashara, huku China ikipinga vikwazo vya teknolojia vinavyowekwa na Marekani.
Wakati huohuo, mapigano nchini Ukraine yameripotiwa kuongezeka baada ya mashambulizi mapya ya ndege zisizo na rubani (drone) kutoka Russia, huku Ulaya ikiendelea kujadili kuongeza msaada wa kijeshi.
Katika Mashariki ya Kati, hali ya usafirishaji wa mafuta kupitia Mlango wa Hormuz inaendelea kuwa hatarini kutokana na mvutano kati ya Washington na Tehran, hali inayoweza kuendelea kuathiri bei na upatikaji wa nishati hiyo duniani.
Kwa ujumla Trump anakwenda China akiwa kwenye mazingira ya diplomasia yenye shinikizo kubwa, ambapo mafanikio yanaweza kuleta utulivu wa kiuchumi duniani, kushindwa kunaweza kuongeza mvutano kati ya mataifa makubwa kiuchumi.