Ripoti hiyo inaonesha jinsi hatua za kisheria zinavyotumika kushughulikia changamoto kama uongo wa kimazingira (greenwashing), fidia za kaboni (carbon offsets) na matumizi makubwa ya nishati katika vituo vya kuhifadhi data.

Ripoti hiyo iliyopewa jina Mabadiliko ya tabianchi Mahakamani: Hali ilivyo, matokeo na yakujifunza ni toleo la nne tangu mfululizo huo uanzishwe mwaka 2017. Inatathmini mwenendo wa kesi, maamuzi ya mahakama na masuala mapya yanayojitokeza katika jitihada za kisheria za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP, Inger Andersen, alisema “Mashauri kuhusu mabadiliko ya tabianchi yamekuwa chombo chenye nguvu duniani kote katika kuendeleza hatua za kukabiliana na changamoto hizo na kuhimiza uwajibikaji.”

Anderson ameogeza kuwa “Kubadilisha mifumo yetu ya nishati, usafiri, makazi na chakula ni jukumu la pamoja kupitia sera zenye ujasiri na zinazozingatia sayansi. Mifumo huru ya mahakama ni muhimu kuhakikisha mabadiliko haya ni ya haki na yenye ufanisi.”

Mwelekeo mzuri

Kwa mujibu wa takwimu za ripoti hiyo, kufikia tarehe 30 Juni 2025, jumla ya kesi 3,099 zinazohusiana na mabadiliko ya tabianchi zilikuwa zimewasilishwa katika nchi 55 pamoja na mahakama na vyombo vya kimataifa au kikanda 24. Hii ni ongezeko kubwa ikilinganishwa na kesi 2,180 mwaka 2022, 1,550 mwaka 2020, na 884 mwaka 2017.

Ingawa kesi kutoka nchi zinazoendelea au nchi za kusini mwa Dunia bado ni chini ya asilimia 10 ya jumla ya mashauri yote, idadi yake inaendelea kukua kwa kasi. Kwa sasa, mashauri haya yanahusisha karibu kila kipengele cha utawala wa tabianchi, yakiwemo yale yanayohusiana na uhifadhi wa viumbe hai na udhibiti wa uchafuzi wa mazingira.

Ripoti hiyo pia inabainisha maamuzi muhimu kutoka kote duniani, ikiwemo uamuzi wa hivi karibuni wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) unaofafanua wajibu wa nchi katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Mahakama nyingi zimeanza kutambua ushahidi wa kisayansi unaoonesha uhusiano kati ya matukio makali ya hali ya hewa na ongezeko la gesi chafuzi.

Wapo wanaopiga

Licha ya kupigwa huku hatua, ripoti hiyo imeonya kuhusu kuongezeka kwa mashauri yanayopinga hatua za tabianchi, yakiwemo yale yanayolenga kupunguza udhibiti wa mazingira au kuzuia uwekezaji katika miradi inayozingatia utunzaji wa mazingira.

Pia imebainisha ongezeko la mashauri dhidi ya wanaharakati, waandishi wa habari, na mashirika ya kiraia wanaopinga miradi yenye utoaji mkubwa wa hewa ukaa.

Kwa mujibu wa UNEP, matokeo ya mashauri haya yanazidi kubadilisha kanuni, sera, na taratibu za kimataifa kuhusu haki ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi, na kusaidia kuweka misingi mipya ya uwajibikaji wa kisera na kisheria.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *