Dar es Salaam. Safari ya mafanikio ya staa wa Bongofleva, Jay Melody, ni ushuhuda hai kuwa katika muziki, kama ilivyo katika maisha, kupotea si mwisho wa safari bali ni sehemu ya kujifunza kabla ya kurejea na nguvu zaidi.

Jay Melody, mkali wa kibao, Nitasema (2023), kwa sasa anatajwa na wengi kuwa miongoni mwa wasanii wakubwa wa Bongofleva, lakini mafanikio hayo hayakupatikana kirahisi kama inavyoweza kudhaniwa.

Alitambulika kwa mara ya kwanza kupitia wimbo wake, Goroka (2018) chini ya mlezi wake wa wakati huo, marehemu Ruge Mutahaba, akiwa sehemu ya kituo cha kulea vipaji cha Tanzania House of Talent (THT).

JA 02

Wimbo huo ulimfungulia milango mingi katika tasnia ya muziki, na punde tu akaja na nyimbo nyingine zilizofanya vizuri kama ‘Namwaga Mboga ‘aliyomshirikisha Nandy, na ‘Mikogo Sio’ akiwa na Dogo Janja.

Hata hivyo, baada ya mwanzo huo mzuri, safari ya Jay Melody ilianza kuyumba kwani nyimbo alizotoa baada ya hapo hazikupata mafanikio yaliyotarajiwa, hali iliyomkatisha tamaa na kumfanya apotee kwenye ramani.

Akiwa anajiuliza anarudi vipi, mnamo 2019, staa huyo akajikuta katika changamoto zaidi kufuatia kifo cha Ruge, mlezi wake, msimamizi wake wa karibu na mtu aliyempa jina la kisanii la Jay Melody.

JA 03

Mashabiki wengi na hata wadau walihisi huo ndio mwisho wa ndoto yake ya muziki, wakiamini asingeliweza kusimama tena bila nguzo hiyo muhimu.

Jay Melody mwenyewe anakiri kipindi hicho kilikuwa kigumu mno, kiasi cha kumpelekea kukata tamaa na hata kutafuta msaada kwa njia tofauti akienda kutazama nyota yake ili kuelewa sababu ya kushuka kimuziki.

Lakini aliamua kusimama tena, akiamini bado ana nafasi katika Bongofleva, na ndipo akaachia wimbo wake, Huba Hulu (2021) uliogeuka kuwa gumzo kubwa nchini na nje ya mipaka, ukimrudisha Jay Melody kwenye ramani ya muziki kwa kishindo.

JA 01

Huba Hulu ulifanya vizuri zaidi ya Goroka na Namwaga Mboga, na kwa wengi, huu ndio ulikuwa utambulisho wao wa kwanza kwa Jay Melody. Baada ya hapo, akaachia mfululizo wa nyimbo zilizothibitisha kuwa kurejea kwake hakukuwa bahati mbaya.

Nyimbo kama Najiweka (2021) na Sugar (2021) zilipata mafanikio makubwa, tunaweza kusema Jay Melody alikuwa amewaka upya, na safari yake ya mafanikio ilikuwa inaendelea kushika kasi.

Kilele cha safari yake kilifika Julai 2022 alipoachia wimbo ‘Nakupenda’, uliogeuka kuwa wimbo mkubwa zaidi wa Bongofleva kwa mwaka huo.

FAC 02

Ni wimbo uliotamba zaidi kwenye majukwaa yote ya kidijitali ya kusikiliza muziki, na hadi sasa unashikilia rekodi kama wimbo wa Bongofleva uliosikilizwa zaidi kwenye Boomplay kwa muda wote.

Mafanikio hayo hayakuwa ya sifa tu, bali pia ya kifedha, kwani Jay Melody alidai kupitia ‘Sugar’ alipata zaidi ya Sh30 milioni ndani ya miezi mitatu, huku ‘Nakupenda’ ikimwingizia Sh200 milioni kupitia show na mauzo ya mtandaoni.

Mwaka huohuo, Nakupenda ulimpatia Jay Melody Tuzo ya Muziki Tanzania (TMA) 2022 kama Wimbo Bora wa Mwaka, ikiwa ni tuzo yake ya kwanza tangu aanze muziki mwaka 2016. Ushindi huo ulikuja miaka miwili tu baada ya kurejea kwake rasmi, na ulikuwa uthibitisho kuwa juhudi zake hazikuwa bure.

Kufanya vizuri kwa nyimbo zake, ikawa rahisi kwake kufikisha wafuasi (subscribers) milioni 1 katika mtandao wa YouTube akiwa ni msanii wa 13 Tanzania kufanya hivyo.

FAC 05

Waliomtangulia Jay Melody, ni Diamond Platnumz, Harmonize, Rayvanny, Mbosso, Zuchu, Alikiba, Lava Lava, Nandy, Marioo, Aslay, Rose Muhando na Jux, mwanachama wa zamani wa kundi la Wakacha.

Akiwa tayari ameachia albamu mbili, Therapy (2024) na Addiction (2025), zote zikiwa na nyimbo 12, safari yake ni funzo kwa wengi kuwa katika muziki na maisha kwa ujumla kuna kupanda na kushuka ila mwisho wa siku bado kuna nafasi nyingi.

Kwa sasa ni kati ya wanamuziki wanaoshirikishwa zaidi, miongoni mwa waliomshirikisha ni Alikiba (Hatari), Rayvanny (Slow), Phina (Manu), Jux (I Need You), Barnaba (Only You), Mabantu (Fala) na Diamond (Mapoz).

Ikumbukwe Billnass alishinda tuzo yake ya kwanza ya TMA baada ya kutoa wimbo wake, Puuh (2022) akimshirikisha Jay Melody ambao ulimuwezesha kushinda kipengele cha Msanii Bora wa Kiume wa Hip Hop 2022.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *