
“Lengo la Urusi ni kuchochea machafuko, kuweka shinikizo la kisaikolojia kwa watu kwa kushambulia miundombinu ya nishati na reli,” Rais Volodymyr Zelensky ameshutumu siku ya Jumatano, Oktoba 8, mbele ya kundi la vyombo vya habari ikiwa ni pamoja na shirika la habari la AFP.
Imechapishwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Katika wiki za hivi majuzi, majira ya baridi kali yalipokaribia, Urusi ililenga vituo vya umeme, gesi, na reli katika maeneo kadhaa ya Ukraine, na hivyo kuzua hofu ya kampeni sawa na ile ya majira ya baridi kali yaliyotangulia, wakati mamilioni ya watu walitumbukizwa gizani kwa muda au kukosa joto.
Rais wa Ukraine amezungumzia haswa “shinikizo kali kutoka kwa mashambulio ya Urusi” kwenye sekta ya gesi, ambayo inaweza kulazimisha Kyiv kuongeza uagizaji. Wakati wa majira ya baridi ya miaka 2024-2025, mashambulizi ya mabomu ya Urusi yalipunguza nusu ya uzalishaji wa gesi ya ndani ya Ukraine. Bw. Zelensky, hata hivyo, amesema ameona “matokeo chanya” kutoka kwa kampeni ya Ukraine ya mashambulizi dhidi ya viwanda vya kusafisha mafuta vya Urusi, ambayo yamesababisha bei ya mafuta kupanda nchini Urusi tangu majira ya joto.
“Uhaba wa mafuta” nchini Urusi
Hivi majuzi Ukraine pia ilishambulia mtambo wa kuzalisha umeme katika eneo la mpaka wa Urusi la Belgorod, na kusababisha kukatika kwa umeme. “Kuhusu mashambulizi yetu ya kina ndani ya Urusi (…), kuna matokeo chanya,” Bw. Zelensky amesema, akimaanisha “uhaba wa mafuta wa hadi 20% ya mahitaji” nchini Urusi. Katika mstari wa mbele, rais wa Ukraine kwa mara nyingine tena amesifu uvamizi ulioongozwa na vikosi vyake katika kukabiliana na mafanikio ya jeshi la Urusi majira ya joto karibu na Dobropillia, akisema kwamba operesheni hii “iliharibu kampeni ya mashambulizi ya Urusi majira ya joto.”
Kulingana na yeye, hali ni “ya wasiwasi” zaidi kwa jeshi la UKraine mashariki mwa nchi, karibu na miji ya Dobropillia na Pokrovsk katika jimbo la Donetsk, lakini pia katika jimbo la Dnipropetrovsk, karibu na Novopavlivka. “Hii ni changamoto yetu inayofuata,” amesema kuhusu mkoa wa Dnipropetrovsk, ambapo jeshi la Urusi liliingia msimu huu wa joto kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa mashambulizi yake nchini Ukraine mnamo 2022.
Ujumbe wa Ukraine nchini Marekani
Mashambulizi ya Urusi yalisababisha kukatika kwa umeme katika majimbo kadhaa ya Ukraine mwishoni mwa juma lililopita na kugonga vichwa viwili vya treni katika kituo kimoja kaskazini mwa nchi hiyo na kusababisha vifo vya watu kadhaa. Urusi, kwa upande wake, ilikabiliwa na mashambulizi mawili ya ndege zisizo na rubani siku ya Jumatatu na Jumanne, kila moja likihusisha ndege zisizo na rubani zaidi ya 200, miongoni mwa mashambulizi makubwa zaidi ya Ukraine tangu mwaka 2022.
Kwa upande wa kidiplomasia, ujumbe wa Ukraine utawasili Marekani “mapema wiki ijayo” kwa majadiliano juu ya uwezekano wa vikwazo, nishati, na ulinzi wa anga wa Ukraine, Rais Volodymyr Zelensky alitangaza Oktoba 9. Katika ukurasa wake wa X, Bw. Zelensky alibainisha kuwa ujumbe huu utaongozwa na Waziri Mkuu Yulia Svyrydenko na mkuu wa masuala ya utawala katika ofisi ta rais, Andriy Yermak. “Suala la kuzuia mali za Urusi pia litajadiliwa na Marekani,” kiongozi huyo wa Ukraine aliongeza.