Kufuatia kilichotokea kwenye “maadhamano haramu” ya Oktoba 29, 2025 na kutaka kujirudia jana Desemba 9, 2025, kiukweli yamesumbua nchi, jana watu wamefunga maduka yao, ni kama nchi ilisimama watu tukiwa roho juu.

Kwa vile maandamano ni haki ya msingi ndani ya katiba yetu, Watanzania wafundishwe kuijua Katiba yao, sheria zao, haki zao na wajibu wao ili kuepuka na kuepusha kile kilichotokea Oktoba 29 na kutaka kujirudia tena jana, Desemba 9.

Haki ya kuandamana ipo kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Ibara ya 18(1), inatamka kuwa “kila mtu ana haki ya kuwa na maoni na kueleza mawazo yake.” Aidha, Ibara ya 20(1) inaeleza kuwa “kila mtu anao uhuru wa kukusanyika kwa amani, kushirikiana na watu wengine, na kwa ajili ya kujadili masuala ya manufaa ya umma na kueleza maoni yake.” Hii ina maana kuwa maandamano ya amani ni haki ya msingi ya kila raia, siyo kosa la jinai.

Sheria ya Jeshi la Polisi na Polisi Wasaidizi (Police Force and Auxiliary Services Act), Sura ya 322, inatoa mamlaka kwa polisi kudhibiti mikusanyiko ya umma yenye viashiria vya uhalifu, lakini haifuti haki ya kikatiba ya kuandamana. Sheria ya Huduma za Vyama vya Siasa (Political Parties Act) pia inatambua haki ya vyama vya siasa kufanya mikutano na maandamano kwa kufuata taratibu. Hivyo basi, haki ya kuandamana haipaswi kuzuiwa kiholela au kwa misingi ya hofu ya kisiasa, ila waandamanaji wafuate katiba, sheria, taratibu na kanuni za maandamano.

Kwa vile maandamano ni haki ya kikatiba kwenye katiba yetu, ila hakuna haki bila wajibu, kwenye kutimiza haki hiyo ya maandamano, kuna wajibu wa kutimiza, kwa anayetaka kuandamana sheria inasema atamtaarifa Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD), kwa maandishi si chini ya saa 48 kabla ya maandamano, akieleza maandamano yatakakoanzia, njia za kupita na kule yatakakoishia ili waandamanaji wapatiwe ulinzi.

Sheria inataka polisi wataarifiwe kwa maandishi ili kutoa ulinzi na jibu la polisi ni kwa maandishi ama kutoa ulinzi kwa waandamanaji, ama kuzuia maandamano, hivyo hilo jibu la polisi ndio linaitwa kibali.

Maandamano yasiyo na barua ni kuandamana kiholela holela bila kutimiza wajibu, bila malengo mahsusi, bila kiongozi, bila njia ya maandamano, bila mwongizo, bila uelekeo maakumu na fujo zinazoandamana na maandamano hayo ni kutokana na kukosekana kwa elimu ya katiba, sheria, haki na wajibu.

Kwenye utetezi wa haki nchini Tanzania, tukubali tukatae, Rais Samia Suluhu Hassan ana nia njema na ya dhati ya kuhakikisha Watanzania wanatendewa haki kwenye vyombo vya utoaji haki, na moja ya udhaifu mkubwa katika utoaji haki Tanzania, ni Watanzania hawazijui haki zao.

Haki hailetwi kwenye kisahani cha chai, haki ni stahili na stahiki inayopaswa kutolewa bila wewe kuiomba, na ikitokea haki haikutolewa au haikutendeka, haki haiombwi, bali inapaswa kudaiwa, sasa ukiwa mtu hujui haki yako, huwezi kudai kitu usichokijua!

Hiki kitu cha Watanzania kutokujua haki zao, nimesikia tena, Rais Samia, akirudia kukisema kwenye kilele cha siku ya sheria iliyoadhimishwa kitaifa uwanja wa Chinangali, jijini Dodoma.

Kwenye hili, Rais Samia alisema: “Wanasema, kuna msemo maarufu kwamba haki hupewi mkononi, lazima uitafute, lakini katika kutafuta haki kuna ujuzi, wananchi wetu wengi hawana ujuzi wa kutafuta haki zao kwa hiyo tuwasaidie kutafuta au kupata haki zao.”

Pia, hii si mara ya kwanza kwa Rais Samia kuzungumzia changamoto ya haki kwa Watanzania wengi wasiojua haki zao, mwaka juzi siku maadhimisho ya miaka 10 ya taasisi ya Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) inayoongozwa na Onesmo Ole Ngurumwa.

Rais Samia alisema: “Mtetezi mkubwa wa haki za binadamu ndani ya Tanzania ni Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo serikali ndiyo inaitekeleza, ndio sheria mama ambayo haki zote za binadamu wanaoishi Tanzania”.

Rais Samia anaendelea, “suala langu kwenu ni “je, hawa wanadamu tunaowatetea, wanaijua hiyo katiba na nataka niache kazi kwenu katika eneo la elimu kwa umma, muifanye kazi hii ya kuwaelekeza watu waijue Katiba yao, kwa sababu wanapodai haki, lazima wajue na wajibu wao, haki ziko kwenye Katiba na wajibu uko kwenye Katiba wakielekezwa vizuri wataujua na wajibu wao nini kikatiba.”

Kile kilichotokea kwenye yale maadhamano ya Oktoba 29, kilitokea kwa sababu vijana wetu wanataka kuandamana kudai haki huku hawajui wajibu wao, kwa sababu hawajawahi kufundishwa popote  jinsi ya kuandamana.

Ukimuangalia Rais Samia na kusikiliza kauli zake katika hili la haki, kusema ukweli kabisa, Rais Samia ana nia ya dhati kutoka moyoni mwake kuhakikisha Watanzania wanatendewa haki na ndio maana akawasamehe wale vijana wetu kwa kuandamana kufuata mkumbo tu huku hawajui watendalo.

Lakini, pia, kitendo cha serikali yetu  kuwapiga risasi za moto waandamanaji wasio na silaha za moto, kiukweli kabisa hakikua sahihi kwa sababu GPO ya Polisi inaelekeza ni wakati gani na mazingira gani polisi watatumia risasi za moto.

Mwalimu Nyerere aliwahi kutuasa kutenda kosa si kosa, kosa ni kurudia kosa. Vijana hawa walitenda kosa la kuandamana na serikali yetu kuwajibu kwa makosa kwa risasi ambazo hazina macho zikawapata waliokuwemo na wasio kuwemo, hakuna ubaya serikali yetu ikakiri kutokea kwa makosa na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama (CDF, IGP na DGIS) walipaswa kukaa pembeni kuipa nafasi Tume ya Uchaguzi iliyoundwa.

Sisi vyombo vya habari ni wadau muhimu sana wa kulisaidia Taifa, hivyo kwanza nitoe pongezi kwa serikali ya awamu ya sita kutushirikisha sisi media. Rais Samia alipolihutubia Bunge jipya la 13, alituzungumzia, amemteua mshauri wa habari, ametuteulia mwanahabari nguli, Tido Mhando kuwa mshauri wake wa habari, ametulia mwanahabari nguli, Bakari Machumu kuongoza Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu,

Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba ametuita kusemezana nasi.

Mkurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, ametuita kusemezana nasi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, ndugu yetu Chalamila ametuita kusemezana nasi, hivyo tuna jukumu la kuielimisha jamii kuhusu katiba, sheria, haki na wajibu wao.

Kila mtu akitimiza wajibu wake kiweledi na kikamilifu, kilichotokea Oktoba 29, kamwe hakijirudii tena.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *