
Kurugenzi Kuu ya Uchaguzi imetangaza matokeo ya awali ya uchaguzi wa wabunge na seikali za mitaa wa Mei 31 usiku wa Juni 4 kuamkia Juni 5, 2026. Uchaguzi ulifanyika katika muktadha wa kipekee, huku kutokuwepo kwa vyama vya kihistoria kama vile UFDG na RPG, ambavyo vilivunjwa mwezi Machi mwaka huu na ambavyo vilitoa wito kwa raia wa Guinea kususia chaguzi hizo. Bila kushangaza, kambi ya rais imeshinda viti vingi katika Bunge la taifa na katika mabaraza ya madiwani.
Imechapishwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Na mwandishi wetu huko Conakry, Tangi Bihan
Idadi ndogo ya wapiga kura ilishuhudiwa katika vituo vya kupigia kura siku ya Jumapili, lakini kiwango cha ushiriki hatimaye kilifikia 53% kwa uchaguzi wa wabunge na 59% kwa uchaguzi wa serikali za mitaa, kulingana na Kurugenzi Kuu ya Uchaguzi nchini Guinea.
Kwa upande wa matokeo, chama cha Mamadi Doumbouya cha Generation for Modernity and Development (GMD) na vyama washirika vimeshinda karibu viti vyote katika Bunge la taifa.
Vyama vya upinzani kama vile Chama cha Democratic Front of Guinea (Frondeg) na kambi ya kiliberali vitalazimika kukubaliana kwa kiti kimoja kila kimoja katika Bunge lenye wanachama 147.
Matokeo kama hayo yameshuhudiwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa: GMD ilishinda wingi kamili au kiasi katika karibu manispaa zote, iwe Conakry au katika miji ya mikoani.
Kulingana na matokeo haya ya awali, hakuna chama cha upinzani ambacho kilishinda katika mji wowote mkubwa wa nchi.
“Kushindwa kwa utendaji kazi”
Hata hivyo, kufanyika kwa uchaguzi huu kunapingwa na baadhi ya vyama vya siasa. Waangalizi kutoka West Africa Network for Peacebuilding (WANEP) wamebainisha katika ripoti yao “kushindwa kwa utendaji kazi” katika upangaji wa kura na hata “kesi zilizothibitishwa za ufisadi, shinikizo na kuingiliwa kwa utawala” katika baadhi ya maeneo.
Kulingana na kanuni za uchaguzi, wagombea kwenye nafasi ya ubunge wana siku nane za kukata rufaa. Wagombea wa uchaguzi kweye nafasi ya madiwani wana siku tatu.
Chama cha Frondeg cha Abdoulaye Yéro Baldé na kambi ya kiliberali ya Faya Millimono watatangaza katika saa zijazo kama watawasilisha rufaa.
Chaguzi hizi mbili zinakusudiwa kuashiria hatua mpya kuelekea kurejea kwa utaratibu wa kikatiba tangu mapinduzi ya mwezi Septemba 2021.