Dar es Salaam. Katika kuendeleza jitihada za kuhamasisha utunzaji wa mazingira na maendeleo endelevu nchini, PASS Trust imeendesha kampeni ya upandaji miti katika Shule ya Sekondari Kisarawe kama sehemu ya utekelezaji wa ajenda yake ya Inclusive Green Growth (IGG).
Kampeni hiyo iliyobebwa na kaulimbiu isemayo: ‘Mti mmoja kwa Mustakabali Endelevu, Kusaidia Jamii Kutunza Ardhi Inayosaidia Maisha na Mustakabali Wao’ iliwakutanisha wanafunzi, walimu, viongozi wa Serikali, wadau mbalimbali pamoja na wananchi kwa lengo la kuhamasisha uwajibikaji wa mazingira na kujenga uelewa wa muda mrefu kuhusu uendelevu.
Mpango huo ni sehemu ya mkakati mpana wa PASS Trust wa kuendeleza shughuli za uhifadhi wa mazingira, ambapo taasisi hiyo inalenga kupanda zaidi ya miti 2,000 ndani ya mwaka huu kupitia kampeni mbalimbali zinazohusisha jamii, vijana pamoja na elimu ya kilimo endelevu.
Akizungumza mwishoni mwa wiki wakati wa hafla hiyo, Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa PASS Trust, Doreen Mangesho, alisema kampeni hiyo inalenga kujenga uelewa wa muda mrefu kwa vijana kuhusu umuhimu wa mazingira na mustakabali wa sekta ya kilimo.
“Leo hatujaja kupanda miti pekee. Tumekuja kupanda uelewa, uwajibikaji na fikra za muda mrefu kwa vijana. Mustakabali wa kilimo unategemea namna tunavyolinda mazingira yetu leo,” alisema.
Alisema PASS Trust ilichagua kufanya shughuli hiyo shuleni kwa makusudi ili kuanza kujenga uelewa wa mazingira kwa kizazi kijacho.
“Tulitaka wanafunzi waelewe kuwa kilimo na utunzaji wa mazingira haviwezi kutenganishwa. Kulinda mazingira ni kulinda maisha, uchumi na fursa za baadaye,” aliongeza.
PASS Trust inaendelea kufanya kazi kwa karibu na wakulima, wafanyabiashara wa sekta ya kilimo pamoja na jamii mbalimbali nchini, huku ajenda ya uendelevu ikiwa sehemu muhimu ya mkakati wake wa Inclusive Green Growth, unaolenga maendeleo yenye ustahimilivu, matumizi bora ya rasilimali, ubunifu pamoja na uwajibikaji kwa mazingira.
Miti ya matunda iliyopandwa katika shule hiyo inatarajiwa kusaidia kuboresha mazingira, kupunguza athari za hewa ukaa, kuongeza uoto wa asili pamoja na kujenga mazingira bora kwa wanafunzi na jamii inayowazunguka.
Mhamasishaji wa vijana, Benson, ambaye pia alishiriki katika shughuli hiyo, aliwahimiza wanafunzi kuwa mabalozi wa utunzaji wa mazingira katika jamii zao.
“Miti tunayoipanda leo inaweza kuonekana midogo sasa, lakini miaka ijayo itanufaisha watu wengi. Vijana wana wajibu mkubwa wa kulinda mazingira kwa ajili ya maisha ya baadaye.”
“Ushirikiano wa namna hii una mchango mkubwa katika kuhamasisha jamii, hasa vijana, kushiriki katika kujenga mazingira endelevu kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho,” alisema.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Kisarawe, Fanuel Nicodemas, aliipongeza PASS Trust kwa kuichagua shule hiyo kuwa sehemu ya kampeni yao, akisema kilichofanyika kimeongeza uelewa wa wanafunzi kuhusu mazingira na uendelevu.
“Zaidi ya kupanda miti, wanafunzi wetu wamepata elimu muhimu kuhusu uhifadhi wa mazingira na umuhimu wake kwa maisha ya baadaye,” alisema.
PASS Trust imeeleza kuwa kampeni hiyo ya upandaji miti itaendelea katika maeneo mbalimbali nchini mwaka mzima kama sehemu ya juhudi zake za muda mrefu za kuhamasisha utunzaji wa mazingira, maendeleo endelevu pamoja na kujenga jamii zenye uelewa kuhusu mabadiliko ya tabianchi na kilimo endelevu nchini Tanzania.
