Dar es Salaam. Benki ya Dunia (WB) imeipongeza Tanzania kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo inayofadhiliwa na taasisi hiyo, ikiitaja kuwa miongoni mwa mataifa yanayoitekeleza kwa ufanisi mkubwa barani Afrika.
Pongezi hizo zimetolewa Jumatatu, Mei 18, 2026 na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia anayemaliza muda wake nchini Tanzania, Nathan Belete, alipokutana na Rais Samia Suluhu Hassan, Ikulu jijini Dar es Salaam.
“Miradi ya Tanzania ndani ya Benki ya Dunia, ni miongoni mwa inayotekelezwa vizuri zaidi barani Afrika. Fedha zinazotolewa kwa Tanzania zinatumika vizuri na kuleta matokeo,” amesema Belete.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan (kulia) akiwa kwenye mazungumzo na aliyekuwa Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia anayesimamia nchi za Malawi, Tanzania, Zambia na Zimbabwe, Nathan Belete (wa tatu kutoka kushoto), Ikulu Jijini Dar es Salaam jana Mei 18, 2026.
Amesema katika kipindi chake cha kazi nchini Tanzania, ushirikiano kati ya Serikali na Benki ya Dunia umeendelea kuimarika katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya, maji, nishati, miundombinu, hifadhi ya jamii pamoja na mageuzi ya kisera.
Aidha, amesema utekelezaji wa miradi visiwani Zanzibar nao umeonyesha mafanikio makubwa kutokana na usimamizi mzuri wa Serikali.
Belete ameyasema hayo alipofika Ikulu kumuaga Rais Samia baada ya kumaliza muda wake wa kazi nchini, sambamba na kumtambulisha mrithi wake, Firas Raad, ambaye tayari ameanza rasmi majukumu yake Tanzania.
Kwa upande wake, Rais Samia amemshukuru Belete kwa mchango wake tangu alipoanza kazi nchini Novemba 2022, akisema ushirikiano wake umeendelea kuimarisha mahusiano kati ya Tanzania na Benki ya Dunia katika kusukuma mbele ajenda za maendeleo.
Pia ametumia nafasi hiyo, kumpongeza Belete kwa uteuzi wake katika nafasi mpya ya kikanda barani Afrika na kumtakia mafanikio katika majukumu yake mapya.
“Tanzania kwa sasa inatekeleza programu na miradi 18 kwa kushirikiana na Benki ya Dunia katika sekta za usafirishaji, nishati, maji, elimu, maendeleo ya miji, hifadhi ya jamii, mageuzi ya kisera na ustahimilivu wa tabianchi,” amesema.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan (katikati) akiwa kwenye mazungumzo na aliyekuwa Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia anayesimamia nchi za Malawi, Tanzania, Zambia na Zimbabwe, Nathan Belete (wa tatu kutoka kushoto), Ikulu Jijini Dar es Salaam jana Mei 18, 2026.
Amesema miradi hiyo imechangia kuboresha maisha ya wananchi huku Serikali ikiendelea kuweka mkazo katika utekelezaji wa vipaumbele vinavyoendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Akitaja baadhi ya maeneo ya vipaumbele, Rais Samia amesema ni pamoja na maendeleo ya miundombinu na mtangamano wa kikanda, hususan Ukanda wa Kati na reli ya kisasa ya SGR inayotarajiwa kuunganisha Tanzania na Burundi pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Maeneo mengine aliyoyataja ni pamoja na nishati safi, kilimo, usalama wa chakula, ustahimilivu wa tabianchi, maji, elimu na hifadhi ya jamii.
Katika hatua nyingine, Rais Samia amemkaribisha Mkurugenzi Mkazi mpya wa Benki ya Dunia nchini, Firas Raad na kumhakikishia ushirikiano wa Serikali katika utekelezaji wa majukumu yake.
Kwa upande wake, Raad amesema amevutiwa na kasi ya maendeleo ya Tanzania, utulivu wa uchumi pamoja na fursa zilizopo katika kukuza uchumi unaozalisha ajira na kupunguza umaskini nchini.
