
Dar es Salaam. Katika familia nyingi za Kiafrika, adhabu za kimwili zimekuwa sehemu ya malezi kwa watoto kwa muda mrefu.
Wazazi na walezi wengi waliamini kuwa viboko ni njia sahihi ya kumrekebisha mtoto anapokosea. Hata hivyo, kadiri nyakati zinavyobadilika na tafiti kuhusu ukuaji wa mtoto kuongezeka, mjadala wa matumizi ya viboko katika malezi unaendelea kushika kasi.
Wapo wanaohoji, je! viboko bado vina nafasi katika malezi ya sasa au kuna njia bora zaidi za kumlea mtoto kwa nidhamu na upendo?
Kuna mtaalamu mmoja wa saikolojia ya watoto, hivi karibuni amesikika akisema kuwa wazazi wengi hutumia viboko wakiamini ndiyo njia bora ya kumfundisha mtoto kutambua jema na baya.
Alisema baadhi ya watoto huonekana kubadilika mara moja baada ya kuadhibiwa, jambo linalowafanya wazazi kuamini kuwa adhabu hiyo inafaa.
Hata hivyo, kwa mtazamo wa nyakati hizo, wazazi wengi walilelewa kwa viboko, hivyo wanaamini ndiyo msingi wa nidhamu.
Lakini wazazi na walezi wa leo, wanapaswa sasa kujiuliza kama mtoto anabadilika kwa kuelewa kosa lake au kwa kuogopa kuadhibiwa kwa kuchapwa viboko.
Kwa upande mwingine, baadhi ya wazazi wanaona viboko vina nafasi ndogo katika mazingira ya sasa ya malezi.
Wiki iliyopita nilizua mjadala nilipokuwa saloon, kuna mama mmoja wa watoto watatu anayeishi Msasani jijini Dar es Salaam, alisema zamani watoto walikuwa na hofu kubwa kwa wazazi, lakini leo watoto wanahitaji zaidi mawasiliano na kuelekezwa kwa utulivu.
Alisema akimueleza mtoto kwa upole na kumuonyesha madhara ya kosa lake, anaelewa zaidi kuliko kumpiga. Alisema viboko vinaweza kumfanya mtoto awe mkaidi au mwenye hofu.
Tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa matumizi ya mara kwa mara ya adhabu za kimwili yanaweza kuathiri afya ya akili ya mtoto.
Watoto wanaopigwa kupita kiasi wanaweza kuwa wakali, waoga, au kupoteza kujiamini. Wengine hujifunza kutumia nguvu wanapotatua matatizo yao kwa sababu wanaamini kuwa nguvu ndiyo njia ya kurekebisha makosa.
Utafiti mdogo nilioufanya, athari hizo huonekana hata darasani, baadhi ya watoto wanaopata adhabu kali nyumbani huwa na ugumu wa kushirikiana na wenzao au kueleza hisia zao kwa uhuru.
Mtoto anayekuzwa kwa vitisho muda mwingine hushindwa kujiamini. Anaweza kuwa mkimya kupita kiasi au mwenye hasira kwa wengine.
Hata hivyo, wapo wanaoamini kuwa kuondoa kabisa viboko kunaweza kuathiri nidhamu ya watoto.
Lakini wataalamu wa malezi wanasema changamoto ya watoto kutowasikiliza wazazi imeongezeka kwa sababu baadhi ya wazazi wameacha kabisa kuwa wakali wanapohitajika.
Wanasema malezi yanahitaji mipaka. Mtoto akijua hatapewa adhabu yoyote akikosea, anaweza kufanya anavyotaka. Wanasema tatizo si viboko pekee, bali namna vinavyotumika.
Wataalamu hao wanasisitza kuwa adhabu yoyote inapaswa kuzingatia utu wa mtoto na isitokane na hasira. Hivyo, mzazi hapaswi kumpiga mtoto kwa lengo la kumuumiza, bali kumkumbusha wajibu na maadili.
Kwa maana nyingine, wazazi wanashauri katika nyakati hizi za sayansi na teknolojia, kutumia njia mbadala za kumrekebisha mtoto badala ya viboko.
Njia hizo ni pamoja na mazungumzo, kumpokonya mtoto baadhi ya vitu anavyovipenda kwa muda, kuweka sheria zinazoeleweka nyumbani, pamoja na kuwa mfano mzuri kwa watoto.
Siku zote tunaambiwa kuwa watoto hujifunza zaidi kupitia tabia za wazazi kuliko maneno.
Ukimtaka mtoto awe mtulivu lakini wewe mzazi una hasira muda wote, mtoto atajifunza hasira. Ikumbukwe kwamba nidhamu inaanza na mzazi mwenyewe.
Hivyo wazazi wanapaswa kutumia muda kuwasikiliza watoto wao na kujenga ukaribu nao. Kwa kufanya hivyo, mtoto hujisikia salama kueleza changamoto zake na huwa rahisi kuelekezwa bila kutumia nguvu.
Katika dunia ya leo yenye mabadiliko makubwa ya kijamii na kiteknolojia, malezi yanahitaji uvumilivu, maarifa na mawasiliano mazuri. Ingawa mjadala kuhusu viboko utaendelea kuwepo, jambo muhimu ni kuhakikisha mtoto anakua katika mazingira salama yanayomjenga kimaadili, kihisia na kiakili.
Mwisho wa yote, wazazi wengi wanakubaliana katika jambo moja kwamba mtoto anahitaji nidhamu.
Tofauti iliyopo ni kuhusu njia bora ya kuifikisha nidhamu hiyo bila kuharibu uhusiano kati ya mzazi na mtoto. Malezi bora si yale yanayojengwa kwa hofu pekee, bali yale yanayochanganya upendo, maelekezo na uwajibikaji.
