Dar es Salaam. Msanii wa filamu anayetamba katika tamthilia ya Jua Kali, Wanswekula Zacharia ‘Dora’ amesema hana muda na wanaomshangaa kutokana na mwonekano wake kwani hawajui alipotoka na mapito aliyopitia.

Aliyasema hayo wakati anazungumza na mashabiki wake live kupitia TikTok.

Dora anasema wakati akiwa mdogo alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa sickle cell, hivyo alikuwa na mwili mdogo zaidi kuliko anavyoonekana sasa.

“Mwili wangu nauona mkubwa kwa sasa. Niliosoma nao shule ya msingi ni mashahidi wakati naanza darasa la kwanza wanafunzi wenzangu walikuwa wanasema katoto kamekuja kusoma, hivyo nikawa mkali sikuruhusu unyonge. Hilo lilinisaidia kujiamini,” anasema Dora.

“Ugonjwa wa sickle cell unaumiza sana, ila anayemeza dawa vizuri akifikisha miaka 18 anaweza akapona kabisa.”

Anasema kuna wakati hataki hata kukumbuka mateso aliyoyapitia wakati anasumbuliwa na changamoto hiyo hadi akafikia hatua ya kutomeza dawa na sasa anajisikia vizuri.

DOR 01

“Nilikuwa siwezi kunywa kitu chochote cha baridi wala kukaa sehemu ya baridi kwa siku nilikuwa nameza dawa nane ili nikae sawa na nilikuwa najisikia maumivu makali,” anasema Dora na kuongeza:

“Kuna siku nilimeza dawa halafu nikatapika sana, nililia kwa uchungu na nilitamka maneno mazito nisiyotamani kuyakumbuka, nilimwambia Mungu kama uliniumba kwa nini nateseka, kama hutaki nifurahi basi nichukue, tangia hapo nikaanza kujisikia vizuri na simezi tena dawa.”

DOR 05

Dora anasema kuna kitu anatamani. “Huku mbeleni natamani kufanya kitu kwa ajili ya kuwatetea watu wenye ugonjwa huo ama kuwasaidia ili kuweza kufikia ndoto zao kama ambavyo nipo mimi kwa sasa. Nipo vizuri na naendelea na majukumu ya kila siku,” anasema.

Dora anasema anatambua ugonjwa huo unatokana na sababu mbalimbali ikiwemo kurithi. “Wapo ambao viashiria vinaonyesha ni ugongwa wa kurithi, nasisitiza watumie dawa vizuri wanapofika umri wa miaka 18 kuna uwezekano wa kupona ili wakiwa wadogo huwa wanasumbuka.”

DOR 04

Msanii huyo umaarufu na muonekano alionao, anaamini kwamba amekuwa mfano wa kuigwa kwa watu wa aina yake, kwani kuna wengine wanashindwa kuzipambania ndoto zao kutokana na kejeli za watu.

“Kwa sasa watu wakinishangaa naona wanamshangaa Dora maarufu na msanii na kuona wamefurahi kumuona na siyo muonekano wangu. Dhihaka kwa sasa hazina nafasi maishani mwangu,”anasema Dora na kuongeza:

“Katika mitandao ya kijamii nikiona anakuja mtu kunishushia heshima nampa ‘bloku’, sitaki nikumbuke mapito yangu ya zamani pia sitaki niwaangushe wanaoniona kama mfano. Wajue tulivyoumbwa siyo kilema hata akiwa mlemavu ana haki ya kuishi na kufurahia maisha.”

DOR 03

Wakati akiendelea kueleza mapito hayo kuna shabiki aliyemuuliza kama ana mpango wa kujifungua na mapito yake hayamtishi kuja kupata mtoto mwenye ugonjwa huo? Alijibu: “Kitu nachohofia ni hicho, lakini namwamini Mungu siwezi kupata mtoto wa aina hiyo. Nitazaa kwa aina yoyote ile lazima niitwe mama, natamani kupata mtoto wa kike na wa kiume na ikiwezekana mapacha.”

Mwandishi wa Mwananchi alipata nafasi ya kumuuliza je, hasumbuliwi na mahusiano na nani alikuwa anamtazama kama mfano wa kuiga nyayo zake na Dora anajibu: “Sisumbuliwi na mahusiano mimi ndiye naacha, kwani siyo vitu nilivyovipa nafasi ya kuninyima amani.

“Msanii namba moja aliyekuwa ‘aikoni’ kwangu Taraji P Henson kutoka Washington, Miriam Ismail na Elizabeth Michael ‘Lulu’ na niliwahi kumwambia nampenda ni shabiki wake toka nikiwa mtoto.”

Shabiki mwingine alimuuliza haonekani katika tamthilia ya Jua Kali, na hapo akajibu: “Bado nipo mtaniona tu, kwani bado inaendelea.”

DOR 02

Anawashauri mashabiki wake wasijikweze kwa vyeo, umaarufu, utajiri au umaskini akisisitiza waishi maisha ya kawaida: “Vitu vyote vinapita kuishi maisha ya kawaida yana raha sana, mimi ni mstaarabu sipendi kusogelewa na watu ambao wanadharau.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *