Serikali imechukua tahadhari ya muda kwa kusitisha utoaji wa vibali vya mikutano ya hadhara kwa vyama vyote vya siasa nchini, ikieleza kuwa hatua hiyo inalenga kulinda amani, usalama wa wananchi na mali zao.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi leo, Ijumaa Juni 26, 2026, amesema uamuzi huo umetokana na kuwepo kwa viashiria vya uchochezi na mipango ya vurugu inayoratibiwa kupitia mikutano ya hadhara na mitandao ya kijamii.
Taarifa za uhakika zinaeleza, baadhi ya mikutano ya kisiasa imekuwa ikitumika kuhamasisha vurugu, uvunjifu wa amani na vitendo vinavyoweza kuhatarisha utulivu wa nchi, hali iliyochangia kuchukuliwa kwa hatua hiyo ya tahadhari.
Katambi, amemwelekeza Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) kutotoa vibali vya mikutano ya hadhara kwa chama chochote cha siasa katika kipindi hiki, huku akisisitiza kuwa wananchi wanapaswa kuendelea na shughuli zao za kiuchumi kwa amani.
Aidha, Serikali imesema itaendelea kuchukua hatua dhidi ya mtu au kundi lolote litakalobainika kupanga au kushiriki matukio ya uvunjifu wa amani, ili kuhakikisha usalama na utulivu vinaendelea kutamalaki nchini.
(Feed generated with FetchRSS)